1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaongeza vituo 800 vya kupiga kura

Hawa Bihoga5 Machi 2019

Tanzania kupitia tume yake inayosimamia uchaguzi imeongeza zaidi ya vituo 800 vya kupiga kura. Hatua hiyo ni sehemu ya uboreshaji wa shughuli za uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3ERuc
Tansania Daressalam Wahlen
Picha: DW/E. Boniphase Amas

Tume ya uchaguzi nchini Tanzania NEC imeongeza zaidi ya vituo mia nane vya kupigia kura ikiwa ni sehemu ya uboreshaji kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. 

Mabadiliko hayo yanakuja kutokana na maelekezo ya sheria ya taifa ya uchaguzi kifungu cha 15 na sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo tume ya uchaguzi inatakiwa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili ndani ya miaka mitano.

Hili limeipa sababu tume ya taifa ya uchaguzi kuongeza idadi ya vituo vya kuandikisha wapigia kura kutoka  36,549 mwaka 2015 hadi vituo 37,407 huku vituo 6,208vikibadilishwa majina na 817 vikihamishwa kutoka eneo moja hadi jingine.

Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Jaji  Semistocles Kaijage amesema kuwa hiyo itatoa fursa kwa wapiga kura wapya kushiriki chaguzi lakini pia imeondoa fursa ya majengo ya vyama vya siasa kutumika kama vituo vya kujiandikishia na kupiga kura.

Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania ​​Semistocles Kaijage
Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania ​​Semistocles KaijagePicha: DW/S. Khamis

Kwa upande wa vifaa kwa ajili ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Jaji Kaijage amesema mchakato wa  kupata vifaa vya kukarabati mashine za BVR umekamilika na kinachofuata ni kuvifanyia majaribio ya  uandikishwaji ambayo yatafanyika katika kata ya kihonda Morogoro na kata ya kibuta mkoani pwani.

Hata hivyo wawakilishi wa vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo na tume ya taifa ya uchaguzi, wamesema kuwa kuongezwa kwa vituo hakutaleta tija katika uchaguzi sababu tume haipo huru na haina watumishi wa kutosha kusimamia taratibu mbalimbali za uchaguzi.

Ikiwa Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu, tayari tume imeshachapisha miongozo mbalimbali kwa wadau, ikiwemo elimu ya mpigakura na maelekezo katika zoezi  la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.