1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi wa mitaa zakamilika Tanzania

26 Novemba 2024

Vyama vya siasa vimetumia dakika za lala salama kurusha turufu zao za mwisho kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho nchi nzima.

https://p.dw.com/p/4nS2G
Wafuasi wa chama tawala CCM wakisikiliza kampeni za uchaguzi
Wafuasi wa chama tawala CCM wakisikiliza kampeni za uchaguziPicha: Ericky Boniphase/DW

Viongozi wa vyama vya siasa wametumia siku ya leo kunadi sera za vyama vyao, kutoa elimu ya mpiga kura  huku wakilia rafu dhidi ya mchakato wa uchaguzi na wagombea wao.

Soma: Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zaanza Tanzania

Msemaji wa ACT Wazalendo anayehusika na  masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Rahma Mwita amelaani vikali matukio ya kutekwa, kukamatwa, na kutishiwa kwa viongozi wa chama hicho saa chache kabla ya uchaguzi.

"Tulisema kama wapinzani na tulisema kama chama, msimamo weru ni kwamba hatuwezi kujiengua, kwamba tutapambana mpaka dakika ya mwisho. Lakini changamoto ni kwamba kila kikiondoka kikwazo hiki kinakuja kingine. Hatuwezi kukubali hili jambo. Kama tumeamua kufuata demokrasia ya vyama vingi, tufuate demokrasia."

Mkurugenzi wa Itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA, John Mrema amesema chama chao kimefanikiwa kufanya kampeni nchi nzima na lakini wakatoa  angalizo kwa serikali.

"Tuseme tu kwamba kwa sasa tunapokwenda kumaliza kampeni hizi, tunatoa wito kwa serikali, kuhakikisha kwamba  haya tunayoyasikia hayatavuruga uchaguzi kesho."

Wafuasi wa vyama vya upinzani vya Chadema na Act-Wazalendo
Wafuasi wa vyama vya upinzani vya Chadema na Act-WazalendoPicha: Ericky Boniphase/DW

Kwa upande wa CCM, wao wameendeleza kampeni zao ambapo Katibu Mkuu wa chama hicho Emmanuel Nchimbi  leo amehitimisha kampeni hizo jijini hapa, eneo la Mbagala, jimbo la Temeke.Upinzani Tanzania walalamika wagombea uchaguzi wa serikali za mitaa kuenguliwa kiholela

Wakati huo huo, Jeshi la polisi  katika taarifa yake iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa atakayesababisha uvunjifu wa amani,kesho,  hataonewa muhali bali atachukuliwa hatua za kisheria.

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(ORTAMISEMI) imetoa mambo 9 ya kuyazingatia kesho wakati wa kupiga kura na kuwataka wananchi kuondoka eneo la kupiga kura mara baada ya kumaliza zoezi hilo.Tanzania: yasema wagombea wa upinzani wanaweza kukata rufaa

Uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kesho Novemba 27 kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utajumuisha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, kata, vitongoji na vijiji kwa Tanzania nzima.