1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yalitaka shirika la WHO litoe maelezo kuhusu ebola

Admin.WagnerD24 Septemba 2019

Tanzania imemtaka muwakilishi wa shirika la afya ulimwenguni WHO atoe maelezo juu ya malalamiko yanayohusiana na maambukizi ya ebola, huku shirika hilo likituhumiwa kwa kutoa chanjo ya ebola kwa mgao nchini Congo

https://p.dw.com/p/3Q93t
Tansania | Dr. Hassan Abbas
Picha: DW/S. Khamis

Tanzania imemuita muwakilishi wa shirika la WHO nchini humo kuhusiana na taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba serikali ilikuwa imekataa kutoa taarifa kuhusu visa vinavyoshukiwa kuwa vya maambukizi ya ebola. Msemaji wa serikali ya Tanzania, Hassan Abbasi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter: Serikali imemuita muwakilishi wa WHO nchini kutafuta maelezo ya kina kutoka kwa shirika hilo kuhusu ripoti zinazosambaa katila vyombo vya habari.

Haya yanajiri wakati shirika la madaktari wasio na mipaka Medicins Sans Frontiers MSF likilituhumu shirika la WHO kwa kutumia mfumo usiofaa wa utoaji chanjo likisema utaratibu wa mgao unaotumika unaruhusu virusi kujitokeza tena katika jamii ambazo tayari ugonjwa huo ulikuwa umetokomezwa na watu kulindwa kutokana na maambukizi mapya.

Shirika la WHO limekanusha madai kwamba linatoa chanjo kwa mgao na badala yake limesema linafanya kazi kwa bidii kama mashirika mengine kuutokomeza kabisa mlipuko wa ugonjwa wa ebola katika Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo. Shirika hilo limesema katika taarifa yake kwamba linashirkikiana na serikali ya Congo kuzifikia jamii nyingi na watu wengi kadri inavyowezekana katika maeneo yaliyoathirika na mlipuko wa ebola na wala halijaweka kiwango wala vikwazo katika utoaji wa chanjo.

Demokratische Republik Kongo | Ebola Epidemie
Wafanyakazi wa afya mjini Goma, mashariki mwa CongoPicha: Getty Images/AFP/P. Tulizo

Shirika la MSF lataka uwazi

Mlipuko wa ugonjwa wa ebola umewaua watu zaidi ya 2,100 tangu katikati ya mwaka uliopita, kiwango ambacho ni cha pili kwa ukubwa tangu mlipuko wa ebola ulipowaua watu 11,300 eneo la Afrika Magharibi kati ya mwaka 2013 na 2016.

Shirika la MSF limetaka pawepo uwazi kuhusu upatikanaji wa chanjo, ambayo inatengenezwa na kampuni la kutengeneza dawa la Marekani, Merck & Co na inayotumika katika kampeni ya shirika la afya duniani WHO ya kukabiliana na ugonjwa wa ebola.

Shirika la WHO na wizara ya afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema tangu mwezi Agosti mwaka uliopita zaidi ya watu 223,000 wamedungwa chanjo dhidi ya ebola ambayo imedhihirika baada ya majaribio kwamba ina uwezo mkubwa wa kuwalinda watu dhidi ya maambukizi. Lakini shirika la Madaktari wasio na mipaka kwa upande wake linakadiria kulingana na idadi ya visa vya maambukizi tangu mlipuko wa ebola, chanjo hiyo inatakiwa iwe imetolewa kwa watu kati ya 450,000 na 600,000, yaani mara mbili.

Maafisa wa afya wa Congo siku ya Jumapili walitoa idhindi kwa mipango ya kutumika aina ya pili chanjo, inayotengenezwa na kampuni ya Johnson & Johnson, kusaidia kupambana na ugonjwa wa ebola.

(rtre, dpae, afpe)