1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yachukuwa uwenyekiti baraza la mawaziri SADC

13 Agosti 2019

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Ndaitwah, alimkabidhi uwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) mwenzake wa Tanzania, Palamagamba Kabudi.

https://p.dw.com/p/3Nojt
Tansania Daressalam Palamagamba Kabudi und Nandi Ndatwah
Picha: DW/H. Bihoga

Akihutubia mawaziri na wawakilishi wa serikali kutoka nchi wananchama wa SADC, Waziri Kabudi alitilia mkazo katika sekta ya viwanda na utalii katika kuimarisha uchumi wa utangamano huo ulioasisiwa kwa malengo ya uhuru wa watu na uchumi kwa mataifa wanachama, miongoni mwa mengine.

Kuongeza kiwango cha ajira kwa vijana, kuimarisha hali ya viwanda na biashara katika utangamano wa nchi hizo kumi na sita, pamoja na kukiongeza Kiswahili katika miongoni mwa lugha rasmi ambazo zinatumika na nchi wananchama ni miongoni mwa ajenda zitazotiliwa mkazo katika kipindi cha mwaka mmoja na baraza la mawaziri katika jumuiya hiyo chini ya uwenyekiti wa Waziri Kabudi, kwa mujibu wa waziri huyo.

Awali kabla ya kumkabidhi uenyekiti huo, Naibu Waziri Mkuu na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Ndaitwah, alilitaka baraza hilo jipya kuhakikisha linajiimarisha katika mabadiliko ya tabianchi pamoja na kujiweka tayari katika kukabiliana na majanga mbalimbali ukizingatia baadhi ya nchi wanachama walikumbwa na vimbunga pamoja na mafuriko yaliyogharimu maisha ya watu na kupotea kwa mali.

Mkutano huo wa baraza la mawaziri ulitarajiwa kufanyika kwa siku tatu, ukitanguliwa na mkutano wa kilele wa SADC kuanzia tarehe 17 Agosti. Miongoni mwa yaliyotazamiwa kujadiliwa ni sera na mikakati ya jumuiya hiyo, ambapo makubaliano yake yangewasilishwa katika mkutano wa wakuu wa nchi kwa ajili ya utekelezwaji zaidi.

Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam