Tanzania: Wakosoaji wa mkataba wa bandari waachiliwe haraka
15 Agosti 2023Watatu hao walikamatwa kati ya Agosti 12 na 13 kwa kuukosoa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai.
Mkataba huo unaweka mfumo wa kisheria wa kuuruhusu Umoja wa Falme za Kiarabu UAE kushirikiana na Tanzania katika maendeleo, usimamizi na uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam pamoja na miundombinu mingine inayohusiana nayo.
"Ukandamizaji wa mamlaka ya Tanzania dhidi ya wakosoaji wa mkataba wa bandari unaonyesha hali ya kutovimilia sauti pinzani. Mamlaka lazima ziwache kuwakamata kiholela wanaharakati kwa sababu tu ya kutoa maoni yao na wanafaa kuachiliwa mara moja, tena bila masharti ili kuhakikisha haki ya uhuru wa kujieleza inaheshimiwa,” ameeleza Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Soma pia: Mwanasiasa mkongwe Tanzania Dokta Wilbroad Slaa anashikiliwa na polisi
Watatu hao, Slaa, Mwabukusi na Nyagali wameukosoa hadharani mkataba wa bandari kati ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai.
Mwabukusi aliwasilisha kesi mahakamani akidai kuwa mkataba huo una vifungu ambavyo vinakiuka katiba ya Tanzania na kwamba unahatarisha uhuru na usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa wakili wake, Slaa alikamatwa na polisi nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam mnamo siku ya Jumapili majira ya saa saba mchana na kupelekwa kwenye kituo cha polisi cha Mbweni. Baadaye, alirudishwa nyumbani kwake ambapo polisi waliikagua nyumba yake na kuchukua baadhi ya vifaa vyake vya mawasiliano. Baada ya upekuzi huo, polisi walimchukua Slaa na kumpeleka kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay.
Wakili wa Mwabukusi na Nyagali ameliambia shirika la Amnesty International kuwa alipokea simu kwamba wanaharakati hao wawili walikamatwa na polisi mnamo siku ya Jumamosi mwendo wa saa tisa alfajiri.
Serikali inajaribu kuzima sauti za upinzani
Kulingana na wakili huyo, wawili hao walikamatwa karibu na mji wa Mikumi, mkoani Morogoro mashariki mwa Tanzania walipokuwa wakisafiri kwenda Dar es Salaam wakitokea Mbeya, kusini magharibi mwa Tanzania.
Emmanuel Masonga, afisa wa chama cha upinzani, pia alikamatwa pamoja na Mwabukusi na Nyagali japo aliachiliwa siku hiyo hiyo na kuagizwa kuripoti katika kituo cha polisi cha Mikumi jana Jumatatu.
Mwabukusi na Nyagali bado wanashikiliwa katika kituo kikuu cha polisi cha Mbeya, baada ya kuhamishwa kutoka Mikumi siku hiyo hiyo. Kulingana na wakili wao, wanaharakati hao wamekataa kula wala kunywa chochote tangu walipokamatwa.
Mnamo AgostI 11, Camilius Wambura, Inspekta Jenerali wa polisi wa Tanzania, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wakosoaji hao wa mkataba wa bandari watakamatwa kwa kauli zao za "uchochezi” zinazoitisha maandamano ya umma kupinga mkataba huo wa bandari.
Soma pia: Mahakama Kuu Tanzania yabariki mkataba wa bandari
Inspekta Jenerali huyo wa polisi amesema kauli za wanaharakati hao zimetafsiriwa kama "kuuchochea umma kuipindua serikali.”
Mawakili wao wameiambia Amnesty International kuwa, wateja wao wamenyimwa dhamana. Kwa mujibu wa mawakili hao, wakuu wa polisi mjini Dar es Salaam na Mbeya wamesema watatu hao watafunguliwa mashtaka ya uhaini japo bado hawajatoa taarifa rasmi juu ya mashtaka hayo.
Kadhalika, upande wa mashtaka pia haujatoa maelezo yoyote juu ya mashtaka yanayowakabili.
Chini ya kanuni ya adhabu ya Tanzania, kosa la uhaini linabeba hukumu ya kifo. Kosa la uhaini pia halina dhamana chini cha kifungu cha 148 cha sheria ya makosa ya jinai.
Mnamo Agosti 10, Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya ilitupilia mbali shauri lililowasilishwa na Mwabukusi na wenzake wanne lililopinga uhalali wa mkataba wa bandari.
Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.