Tanzania: Ripoti ya CAG yazusha joto bungeni
11 Aprili 2023Baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuonesha kuchukizwa na ufisadi uliobainika alipopokea ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini humo hivi karibuni, baadhi ya wabunge wameeleza kushangazwa na mamlaka husika kushindwa kuwachukulia hatua wale wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Soma pia: Rais Samia akosowa mfumo wa utoaji haki
Matamshi ya wabunge hao wameyatoa leo hii jijini Dodoma ambako kumeanza mkutano wa kumi na moja wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania huku bunge hilo likipitisha azimio lake la kumpomgeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya katika uongozi wake.
Wakichangia katika azimio hilo baadhi ya wabunge akiwemo mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka ameeleza kushangazwa na mamlaka husika kushindwa kuwachukulia hatua wale wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kufuatia ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali aliyoiwasilisha hivi karibuni kwa Rais Samia.
Soma pia: Tanzania yasaini mkataba wa reli wa dola bilioni 2.2 na China
Akihutubia mara baada ya kupokea ripoti ya taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU na ile ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, CAG, Rais Samia alionesha kuchukizwa na ufisadi katika sekta mbalimbali ulioibuliwa katika ripoti hiyo.
Kulingana na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wanasema kuwa ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambayo imebaini ufisadi katika baadhi ya taasisi za umma ikiwemo katika baadhi ya halmashauri nchini humu, unathibitisha kuwa hali sio nzuri katika suala zima la uadilifu hasa kwa watumishi wa umma waliopewa mamlaka wameendelea kutumia nafasi zao kupora mali za umma.
Akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka 2021/22 , CAG Charles Kichele alisema shilingi bilioni 11.7 hazikuwekwa katika akunti za benki na wakusanyaji wa mapato kutoka mamlaka za serikali za mitaa 98 nchini huku ripoti hiyo ikibaini matumizi mabaya ya madaraka na kupendekeza tume huru ya kuchunguza matumizi mabaya ya ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), akisema pamoja na mengineyo, fedha zilizotaifishwa kupitia utaratibu wa Plea Bargaining, ziliwekwa kimakosa katika akaunti ya makubaliano ya hiari, badala ya akaunti ya utaifishaji mali.