1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania na Burundi zajadili kuukabili uhalifu.

11 Oktoba 2019

Mkutano wa pamoja wa wakuu wa majeshi ya Polisi kati ya Tanzania na Burundi unafanyika mkoani Kigoma magharibi mwa Tanzania kwa lengo la kupanga mikakati ya kudhibiti uhalifu na ugaidi. 

https://p.dw.com/p/3R7gb
Simon Sirro Polizei Dar es Salaam Tansania
Picha: DW/S. Khamis

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganda alipofungua mkutano huo wa wakuu wa Polisi Burundi na Tanzania amesema Kigoma ni moja kati ya mikoa yenye usalama mdogo kutokana na mwingiliano wa kijamii kati ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo wahalifu hutumia ujirani kufanya uhalifu.

Maganga amesema ushirikiano wa vyombo vya ulinzi kati ya Tanzania na Burundi umefanikisha kudhibiti matukio mengi ya ujambazi unaovuka mipaka na kusema wahalifu wa pande zote mbili wamedhibitiwa.

Burundische Flüchtlinge fliehen vor Gewalt und den politischen Spannungen Burundis nach Tansania
Wakimbizi wa Burundi wametakiwa kufuata taratibu ua kiusalama wanapoingia Tanzania kufanya kazi za vibarua.Picha: AP/J. Delay

Mkuu huyo wa mkoa pia ametoa tamko la kuruhusu raia wa Burundi wanaokuja kufanya kazi za vibarua mashambani nchini Tanzania kufuata taratibu za uhamiaji lakini pia amewaonya watanzania kutowadhulumu maana dhuluma ni moja ya sababu za kuongezeka kwa visa vya ujambazi wa visasi.

Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania IGP Simon Sirro amelishukuru jeshi la Burundi kwa kufanikisha operesheni za pamoja ambazo zimewezesha kukamatwa au kuuawa kwa majambazi katika eneo la mpakani. Jeshi la polisi la Burundi limeipongeza serikali ya Tanzania kwa kutoa mchango mkubwa katika uimarishaji wa usalama nchini Burundi pamoja na kuhifadhi wakimbizi

Mwezi April mwaka huu wakuu wa Polisi Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania walitiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kiintelijensia wa kuimarisha ulinzi mipakani, kubadilishana taarifa pamoja na wahalifu lakini pia kufanya operesheni za pamoja.