Tanzania: Mafuriko yawaua watu 14 Lindi
29 Januari 2020Jumla ya watu 14 wameripitiwa kufariki Dunia Mkoani Lindi, nchini Tanzania kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na idadi hiyo ikitwajwa kuweza kuongezeka kutokana na baadhi ya watu kushindwa kuokolewa, huku msaada mkubwa wa kibinadamu ukihitajika Mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema juhudi za vikosi vya uokoaji zinaendelea ambapo watu 1,531 wameokolewa kati ya wakazi 15,000 wanaodaiwa kuathirika na mafuriko hayo.
Zambi amesema hali si nzuri na uokoaji unaendelea katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko.Mafuriko Wilayani Kilwa Mkoani Lindi yametokea kwenye vijiji vya Kilanjelanje, Nanjilinji A, Ruatwe, Njinjo, Nakiu na Nanjilinji B ambavyo vimezingirwa na maji.
Naye kamishna wa operesheni na mafunzo wa jeshi la Polisi nchini Liberatus Sabas amesema hali si shwari na unahitajika msaada kwa wananchi wa maeneo hayo kama chakula na mavazi.
Wakizungumzia maafa yaliyowakumba baadhi ya wananchi hao wamedai kupotelewa na wazazi na ndugu zao, nyumb zao kubomoka pamoja na kuharibu samani za ndani.
Mafuriko hayo yanatokea ikiwa ni siku chache tu kupita tangu kutolewa kwa taarifa na mamlaka ya hali ya hewa (TMA) nchini iliyotoa tahadhari ya kunyesha kwa Mvua kubwa katika baadhi ya Mikoa ikiwemo ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.