Tamasha la Olimpiki kufunguliwa London
23 Julai 2012Uwanja wa michezo wa Olimpic na kituo cha vidimbwi vya kuogolea katiaka upande wa Mashariki mwa London, vitakuwa mwenyeji wa mashujaa wa Beijing, Usain Bolt na Michael Phelps, ambao walirarua vitabu vya kumbukumbu katika mashindano ya mwaka wa 2008.
Katika upande mwingine wa mji, Roger Federer, Novak Jokovic na Serena Williams watagonga vichwa vya habari wakati Wimbledon ikiwakaribisha miamba hao wa mchezo wa tennis. Aidha kutakuwa na voliboli ambayo maarufu huchezewa ufukweni lakini sasa italetwa katikati ya London, huku uwanja wa Wembley ukiandaa fainali ya kandanda.
Katika uwanja wa riadha, Bolt ambaye ni bingwa mara tatu wa dhahbu katika michezo ya Olimpiki kwenye mbio za mita 100, 200 na 100 za wachezaji wanne wa kupokezana vijiti, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mwenzake wa Jamaica, Yohan Blake, katika fainali ya mbio za mita 100 mnamo tarehe 5 Agosti. Bolt anashikilia rekodi ya ulimwengu ya sekunde 9.58, lakini Blake ni bingwa wa Ulimwengu na ambaye ana muda wa kasi zaidi msimu huu, kutokana na majaribio ya mwezi jana nchini Jamaica.
Nyota wengine wa riadha ni pamoja na mkenya, David Rudisha wa mbio za mita 800, Kenenisa Bekele ambaye alikuwa bingwa wa mbo za mita 5,000 na 10,000 mjini Beijing. Mjini London, hali ya usalama imeimarishwa jinsi anavyoeleza Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, James Brokenshire
Kumbukumbu ya mashambulizi ya Munich
Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Jacques Rogge, leo ameongoza hafla ya kusalia kimya kwa dakika moja kama kumbukumbu ya miaka 40 ya mashambulio mabaya dhidi ya wanariadha wa Israel katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 1972 mjini Munich. Rogge, ambaye alisema hakutakuwa na dakika moja ya kusalia kimya katika sherehe za ufunguzi siku ya Ijumaa, ameiongoza hafla hiyo kuwakumbuka wanariadha 11 wa Israel walioshambuliwa na wanamgambo wa Palestina wakati alipozuru eneo la makaazi ya wanariadha. Alisema ana matumaini makubwa kwamba usalama mjini London umekwekwa katika hali ya juu
Katika habari nyingine za Olimpiki, ni kuwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, imempa kibali mwanariadha wa mbio za marathon, mzaliwa wa Sudan Kusini, ashiriki michezo hiyo chini ya bendera ya Olimpiki katika mashindano hayo ya London.
Guor Marial ambaye ana makao yake nchini Marekani, ambaye ni mkimbiaji wa zamani kushiriki kama mwanariadha huru. Marial aliliambia shirika la habari la AP kuwa sauti ya Sudan Kusini hatimaye imesikika. Alisema hata ingawaje hatabeba bendera ya nchi hiyo katika michezo ya olimpiki, nchi yenyewe imewakilishwa. Marial hana paspoti na hawakilishwi na kamati ya kitaifa ya Olimpiki. Sudan Kusini ilitangaza uhuru wake kutoka kwa Sudan na bado haitambuliwi na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa.
Aboutrika kutegemewa na Misri
Mohamed Aboutrika huenda anaendelea na mazoezi yake ya michezo ya Olimpiki,lakini jana alifunga bao katika dakika za mwisho na kuisaidia Al Ahly kuwabwaga mahasimu wake wakali Zamalek bao moja kwa sifuri katika mchuano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kiungo huyo nyota Aboutrika, ambaye ni mmoja wa wachezaji watatu wenye umri mkubwa waliojiunga na timu ya Misri ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 katika michezo ya Olimpiki mjini London, alirejea mjini Cairo kutoka Ulaya kwa mchuano huo wa siku ya pili. Mchuano huo ulichezewa katika uwanja wa kijeshi wa Cairo ambao haukuwa na mashabiki kwa mara ya kwanza katika uhasimu uliodumu miaka 101.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri: Miraji Othman