1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yazuia wanawake kusafiri pake yao.

28 Machi 2022

Utawala wa Taliban nchini Afhanistan umeyaagiza mashirika ya ndege nchini humo kuwazuia wanawake kusafiri labda tu wakiwa wanasindikizwa na ndugu zao wa kiume.

https://p.dw.com/p/497df
Afghanistan Taliban l Schaufensterpuppe
Picha: Allauddin Khan/AP/picture alliance

Katika hatua hii ya karibuni, Taliban imeyaagiza mashirika ya ndege ya Ariana na Kam kuwazuia wanawake kusafiri hadi pale wanatakapokuwa wanasindikizwa na ndugu zao wa kiume ama  watu wasioweza kuolewa nao "mahram".

Kulingana na maafisa wa anga waliozungumza na shirika la habari la AFP, uamuzi huo umechukuliwa baada ya mkutano uliofanyika Alhamisi iliyopita kati ya wawakilishi wa Taliban, mashirika hayo mawili ya ndege na mamlaka za uhamiaji nchini humo. Wanawake hawaruhusiwi kusafiri peke yao kwa ndege za ndani ama za kimataifa.

Soma Zaidi: Taliban: yaweka zuio la kusafiri

Msemaji wa wizara inayoshughulikia masuala ya kidini na utu ya Taliban hata hivyo alikana madai kwamba mashirika hayo ya ndege yamezuiwa kusafirisha wanawake peke yake, ingawa mawakala wawili wa usafiri wa ndege  waliozungumza na AFP wamethibitisha kuagizwa kuacha kutoa tiketi kwa wanawake peke yao.

Haikuwa wazi iwapo agizo hilo pia litawahusu wasafiria wa kigeni, ingawa mashirika ya ndani ya habari yameripoti kwamba wiki iliyopita mwanamke mmoja wa Kiafghani mwenye pasi ya kusafiria ya Marekani alizuiwa kusafiri.

Afghanistan | Bäckerei in Kabul spendet Brot
Kulingana na maagizo ya serikali, wanaume na wanawake hawatakiw kukutana sehemu moja. Picha: Ali Khara/REUTERS

Taliban yasema hizo ni amri za Mungu na si za serikali.

Mbali na zuio hili, sasa wanawake na wanaume hawatakiwi kutembelea kwa siku moja bustani zilizoko Kabul. Wanawake sasa wanaruhusiwa kutembelea bustani hizo siku za Jumapili, Jumatatu na Jumanne, wakati siku zilizosalia zitakuwa kwa ajili ya wanaume, hii ikiwa ni kulingana na wizara hiyo.

Serikali ya Taliban ya msimamo mkali wa Kiislamu tayari imeanzisha hatua kadha wa kadha zinazobinya uhuru na hasa zinazowalenga wasichana wa Afghanistan na wanawake na kama haitoshi jana Jumapili iliviagiza vituo vya televisheni vya ndani kuacha kurusha taarifa za habari za shirika la habari la Uingereza, BBC.

Taliban ordnen die Schließung von Mädchenoberschulen in Afghanistan an
Baadhi ya wanafunzi wa kike wakirudi nyumbani mara baada ya serikali kutangaza kuzifunga shule za wasichana.Picha: Ahmad Sahel Arman/AFP/Getty Images

Baada ya kurejea madarakani, Taliban waliahidi kulegeza misimamo iliyoitumia enzi ya utawala wao uliodumu tangu mwaka 1996 hadi 2001 ingawa wameanza tena kurejesha misimamo ileile, ambayo ilianza kutumia na watawala wa mikoa kadhaa.

Soma Zaidi: Taliban watoa amri ya kuheshimu haki za wanawake

Wanawake kwa kiasi kikubwa wanazuiwa kuwa sehemu ya maisha ya kawaida. Wanazuiwa kwenda shule na hata kufanya kazi za serikali na kuagizwa kuvaa kulingana na namna kitabu kitakatifu cha Kiislamu cha Quran kinavyoagiza.

Imesema, haya sio maagizo ya jamhuri hiyo ya kiislamu, bali ni ya Mungu kwamba wanaume na wanawake ni watu wasiojuana na kwa maana hiyo hawatakiwi kukutana katzika eneo moja, alisema Mohammad Yahya, afisa wa wizara hiyo alipozungumza na AFP.

Zuio hili jipya kwa wanawake pia linatolewa baada ya Jumatano iliyopita serikali kutangaza kuzifunga shule zote za wasichana za upili, masaa kadhaa baada ya kufunguliwa kwa mara ya kwanza tangu Agosti mwaka jana iliporejesha mamlaka, hatua iliyoibua ukosoaji mkubwa wa kimataifa.

Mashirika: AFPE