Taliban yaahidi ulinzi zaidi misikiti ya Washia
16 Oktoba 2021Ahadi hiyo imetolewa wakati mamia ya watu walikusanyika leo kuwazika wahanga wa shambulizi hilo la kujitoa muhanga lililotekelezwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS ambalo ni la pili katika kipindi cha wiki moja.
Kundi la IS la waislamu wa itikadi kali ya Sunni limedai kuhusika na shambulizi hilo kwenye msikiti wa Fatima katika jimbo la Kandahar ambako washambuliaji wa kujitoa muhanga waliwaua walinzi na kisha kujiripua kwenye kundi la mamia ya waumini wakati wa sala ya Ijumaa.
Afisa mmoja wa Afya amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema idadi ya waliokufa imepindukia watu 41 na wengine 70 wamejeruhiwa huku idadi hiyo inaweza kuongezeka.
"Baadhi ya waliojeruhiwa wako kwenye hali mahututi na tunajaribu kuwahimisha kwenda mjini Kabul" amesema afisa huyo.
Wahanga wa shambulizi hilo wazikwa
Mapema leo Jumamosi makundi makubwa ya watu walijitokeza kuwazika wahanga wa mkasa huo kwenye kaburi la pamoja katika mji wa kusini wa Kandahar.
Mkuu wa polisi wa mji wa Kandahar amesema vikosi kadhaa vitaamriwa kuilinda misikiti yote ya Washia ambayo tayari inapatiwa ulinzi na makundi ya watu wa kujitolea yaliyopewa kibali maalumu cha kubeba na kutumia silaha.
"Kwa bahati mbaya hawakuweza kulilinda eneo hili na katika siku zijazo tutatoa jukumu kwa walinzi maalumu kutoa ulinzi kwa misikiti na madrasa" imesema taarifa ya Taliban iliyochapishwa kwenye msemaji wa kundi hilo kupitia ukurasa wa Twitter.
Shambulizi kwenye msikiti wa Fatima ambao ni msikiti mkubwa zaidi wa Washia huko Kandahar limetokea kiasi wiki moja baada ya shambulizi jingine kama hilo kuulenga msikiti mwingine kwenye mji wa kaskazini wa Kunduz na kuwaua watu wasiopungua 80.
Mashambulizi dhidi ya Washia yautia doa utawala wa Taliban
Mashambulizi dhidi ya misikiti ya Washia na maeneo mengine yanayofungamanishwa na jamii ya wachache ya Hazara, ambayo ina waumini wengine zaidi wa kishia nchini Afghanistan yalikuwa jambo la kawaida chini ya serikali iliyopita iliyokuwa ikiungwa mkono na mataifa ya magharibi.
Kuendelea kutokea kwa mashambulizi ya aina hiyo hata baada ya kundi la Taliban kuchukua udhibiti nchini Afghanistan kumezusha fadhaa kubwa. Matukio hayo yameutia toa utawala wa Taliban unaojinasibu kuwa vuguvugu laolimeleta amani nchini Afghanistan baada ya miongo kadhaa ya vita.
Tangu Taliban walipoikamata Afghanistan mnamo mwezi Agosti, kundi la IS limefanya hujuma kadhaa, tangu mashambulizi madogo hadi makubwa mfano wa shambulizi la siku ya Ijumaa dhidi ya msikiti wa huko Kandahar unaofahamika pia kama msikiti wa Imam Bargah.
Kundi la IS ni madhehebu ya Sunni wanawaona Washia kama waumini wanaokufuru, lakini pia ni wapinzani wakubwa wa kundi la Taliban linaoongoza serikali mjini Kabul, licha ya kuwa wote ni waislamu wa madhehebu ya Sunni.