1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban waitaka Pakistan kukataa misaada ya kiutu

11 Agosti 2010

Watoa shutuma kwa Viongozi wala rushwa kunufaika zaidi

https://p.dw.com/p/OiJM
Eneo kubwa la Pakistan limefunikwa na maji,kama linavyoonekana kwa juu. Pakistan inakabiliwa na upungufu wa misaada ya kiutu.Picha: AP

Wafuasi wa kundi la Taliban,wameitaka Serikali ya Pakistan kukataa misaada inayotolewa na nchi za magharibi kwa ajili ya waathiriwa wa maafa ya mafuriko kwa kueleza kuwa misaada hiyo itatumiwa na viongozi wachache wala rushwa, na kushindwa kuwafikia wahanga wa maafa hayo.

Maafa hayo hadi sasa yamesababisha vifo vya raia 1,600 na wengine milioni 2 kuyahama makazi yao, huku ikielezwa kuwa watu zaidi ya milioni 14 hawana makaazi kufuatia mafuriko yanayoendelea kuikumba nchi hiyo.

Tamko hilo limetolewa katika kipindi ambacho serikali ya Pakistan inahangaika kupata misaada ya kiutu, ambapo msemaji wa kundi la Taliban, Azam Tariq, akizungumza kutoka mafichoni kwa njia ya simu, ameonya kuwa viongozi wa serikali jijini Khyber -Pakhtunkwa na maeneo ya katikati ya jiji hilo, wataitumia misaada hiyo kujinufaisha binafsi.

Ameeleza kuwa viongozi hao, aliowaita kuwa ni wala rushwa na wabinafsi, wamejipanga kuchukuwa fedha za misaada kwa ajili ya kujiwekea katika akaunti zao za binafsi, na kuwaacha wahanga wa misaada hiyo wakiendelea kuteseka.

Naye mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa, Jean Maurice Rippert, ameonyesha wasiwasi wake kuwa tukio hilo la maafa linaweza kutumiwa na baadhi ya vikundi vya uasi kujiimarisha zaidi katika kipindi ambacho serikali inazingatia zaidi suala la maafa hayo, na kuondoa kipaumbele chake katika vita dhidi ya ugaidi.

Imeelezwa kuwa taasisi mbalimbali za Kiislamu zinazohusishwa na mafungamano na makundi ya kigaidi zimekuwa zikikusanya fedha kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo ambayo Umoja wa Mataifa umeielezea kuwa maafa hayo ni makubwa mno kuikumba nchi hiyo, na ambapo itahitaji mabilioni ya dola ili kuweza kuijenga upya miundo mbinu iliyoharibiwa na mafuriko hayo.

Benki ya dunia nayo imeonya kuwa nchi hiyo itapoteza zaidi ya asilimia 4.5 ya pato la taifa, ambapo Rais wa nchi hiyo, Asif Ali Zardari, mume wa aliyekuwa waziri mkuu, Hayati Benazir Bhutto, akikosolewa kwa uamuzi wake wa kuendelea kuwa nje ya nchi wakati maafa hayo yakiendelea nchini mwake.

Zardari,ambaye umaarufu wake umeshindwa kufikia kiwango cha aliyekuwa mkewe, Benazir Bhutto, aliyeuawa kwa kupigwa risasi, alirejea nchini humo siku ya jumanne, ambapo maafisa wa serikali nchini humo wameshindwa kuthibitisha kuwa Rais huyo anaweza kutembelea eneo lililokumbwa na maafa hayo.

Wakati huo huo, wahanga wa maafa hayo wameeleza kuwa wataanza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan pasina kuelewa kuwa watafuturu nini, ambapo umoja wa mataifa umeelezea wasiwasi wake kuwa wananchi wengi wataathiriwa kiafya kutokana na kukumbwa na uhaba wa chakula.

Pakistan ina waumini wengi wa dini ya kiislamu wanaofikia milioni 165, ambapo mmoja wa waumini hao, Nasrat Shah, ameeleza kuwa ataendelea kufunga mwezi wa Ramadhan katika kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na maafa, na kusisitiza kuwa imani yake haiwezi kutikiswa na matukio hayo.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/RTRE

Mhariri: Miraji Othman