Taliban lasema litajibu kwa mashambulizi
13 Mei 2020Taliban limeonya kuwa litajibu kwa mashambulizi iwapo serikali ya Afghanistan itaanza tena kufanya operesheni dhidi yake. Hii ni kufuatia mashambulizi ya Jumanne ambayo serikali imesisitiza kuwa yaliketekelezwa na kundi hilo huku rais Ashraf Ghani akisema vikosi vya Afghanistan vitaanza tena kuchukua hatua dhidi ya Taliban na makundi mengine ya Kigaidi.
Ghani amelishtumu kundi hilo kwa kutekeleza mashambulizi ya Jumanne dhidi ya hospitali ya kina mama wajawazito katika mji mkuu Kabul liliosababisha vifo vya watu 24 wakiwemo watoto wadogo na wauguzi. Kadhalika siku hiyo hiyo watu wapatao 25 waliokuwa wakihudhuria mazishi waliuawa katika shambulio mashariki mwa nchi hiyo.
Kundi linalojiita dola la Kiislamu IS limedai kutekeleza shambulio dhidi ya waombolezaji lakini hadi sasa hakuna kundi limedai kuhusika na shambulio dhidi ya hosiptali. Wizara ya afya nchini humo imesema leo kuwa idadi ya waliofariki katika shambulio la hospitali sasa imefikia watu 24 na majeruhi 16.
Msemaji wa serikali ya Afghanistan Sediq Sediqqi amesema serikali kamwe haitokubali kwamba mashambulizi ya jana hayakutekelezwa na Taliban. Hatahivyo Taliban wamekanusha kuhusika katika mashambulizi hayo.
Rais Ghani alisema vikosi vitachukua tu hatua za kujilinda bila kuwashambulia Taliban kama moja ya ahadi ya upande wa serikali yake kuheshimu makubaliano kati ya kundi hilo na Marekani huku serikali yake pia ikitarajia kuanza majadiliano ya moja kwa moja na Taliban.
Tangu kufikia makubaliano kati ya Marekani na Taliban mnamo Februari, Taliban imejiepusha kwa sehemu kubwa kufanya mashambulizi dhidi ya Kabul. Moja ya vipengee vya makubaliano kati ya Taliban na Marekani ni vikosi vyote vya Marekani na vya kigeni kuondoka kutoka ardhi ya Afghanistan katika mwaka ujao.
Hatahivyo, kutokana na hali tete iliopo kwa sasa, kuna khofu ya kuvurugika kwa mchakato wa amani kusuluhisha mgogoro kati ya Taliban na serikali ya nchi hiyo.
Katika taarifa yake mara baada ya mashambulizi hayo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alitoa wito kwa Taliban na serikali ya Afghanistan kushirikiana kuhakikishia kuwa kuna utendaji wa haki na kuwaadhibu wahusika wa mahambulizi
Mjumbe maalumu wa Marekani nchini Afghanistan Zalmay Khalizad amezitaka Taliban na serrikali ya Afghanistan kushirikiana katika kuleta amani nchini humo.
Vyanzo: AFPE/ DPAE/RTRE