Taifa la Iran sasa ladhibiti waziwazi vyombo vya habari
12 Julai 2012Serikali ya Iran imevionya vyombo vya habari juu ya uchapishaji na utangazaji wa taarifa zinazohusiana na athari za vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya magharibi, huku ikiviomba vyombo hivyo kushirikiana na serikali hiyo ili nchi isiumie.
Onyo hilo tata la serikali inayoongozwa na Mahmud Ahmadinejad limechapishwa katika magazeti ya nchini Iran jana.
Magazeti hayo yamemnukuu Waziri wa Utamaduni na Maongozi ya Kiislamu, Mohammad Hosseini, akisema " Nchi yetu haiwezi kuruhusu vyombo vya habari kuchapisha taarifa yoyote au uchambuzi ambao hauko kwa maslahi ya utawala na taifa kwa ujumla.
Tamko hilo limetolewa na wizara yenye dhamana ya kusimamia vyombo vya habari vya magazeti na tovuti rasmi za habari.
Kauli hiyo ya Hosseini iliyochapishwa kwa mara ya kwanza katika tovuti ya serikali ya dolat.ir ilidai kwamba hali kuhusiana na vikwazo vya mataifa ya magharibi na misukumo mingine hususan katika masuala ya uchumi, yanahitaji ushirikiano na vyombo vya habari ili nchi isiingie matatizoni.
Akifafanua zaidi katika taarifa hiyo mtandaoni, waziri huyo wa utamaduni na maongozi ya Kiislamu amesema, serikali iko mbioni kufanya mkutano na vyombo vya habari inavyovimiliki pamoja na maofisa wa sekta ya uchumi ili wapate taarifa zaidi kuhusiana na mambo muhimu yanayoendelea nchini Iran kwa sasa hususan juu ya vikwazo hivyo, na hivyo kuwa na tahadhari na kuweka maslahi ya taifa mbele.
Vyombo vya habari vinafuatiliwa kwa karibu sana nchini Iran na mara kwa mara mamlaka za serikali hutoa maonyo makali kwa vyombo hivyo juu ya uchapishaji wa taarifa hasi hasa hasa kuhusiana na masuala ya kijamii na kiuchumi, lakini hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu kutumia athari za vikwazo vya nchi za magharibi kuhalalisha udhibiti wa serikali hiyo kwa vyombo vya habari nchini humo.
Onyo hilo linafuatia hatua ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuiwekea Iran vikwazo vya kusafirisha nje mafuta, hatua iliyochangia kushuka kwa kiwango cha mauzo ya nje ya mafuta ghafi, biashara ambayo huipatia Jamhuri hiyo ya Kiislamu theluthi mbili ya mapato yake ya fedha za kigeni.
Tangu mwaka 2010 Iran inakabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi kutoka mataifa mbalimbali kutokana na kuendelea na mpango wake tata wa kinyuklia, ambao mataifa ya magharibi yanaamini unalenga kutengeneza silaha ya kinyuklia, licha ya Iran kukanusha mara kadhaa.
Vikwazo hivyo vinazilenga sekta nyeti za benki na mafuta, ambazo nchi ya Iran inazitegemea pakubwa kwa mapato yake ambayo ndiyo uti wa mgongo wa taifa.
Hata hivyo, propaganda ya serikali hiyo inadai kuwa vikwazo hivyo havina athari yoyote kwa ukuaji wa taifa hilo na kwamba hali ni nzuri tu nchini humo.
Na kutokana na propaganda hiyo, vyombo vingi vya habari vinaepuka kuchapisha taarifa sahihi au takwimu halisi kuhusiana na matokeo ya vikwazo hivyo kwa taifa la Iran. Lakini hata hivyo, wakati mwingine vyombo hivyo hivyo huwanukuu viongozi wa biashara wakitoa matamshi ambayo yanadhihirisha kwamba vikwazo hivyo vinaiathiri nchi hiyo.
Mwandishi: Pendo Paul/AFP
Mhariri:Josephat Charo