1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taasisi za Fedha zidhibitiwe kwa Kanuni na Masharti makali

23 Machi 2010

<p>Je,walipa kodi pekee ndio wabebe gharama za kurekebisha madhara ya mzozo wa fedha uliosababishwa kwa sehemu kubwa na taasisi za fedha duniani?

https://p.dw.com/p/MZre

Hiyo ni madaa kuu katika magazeti ya Ujerumani leo Jumanne. Tataanza na gazeti la "STUTTGARTER NACHRICHTEN" linaloandika:

"Ukuaji wa uchumi umeanguka na mataifa mengine yanakabiliwa na hatari ya kufilisika kwa sababu ya mzozo wa fedha duniani. Sasa pendekezo la kuyataka mabenki kutoa sehemu ndogo ya mapato yake kuanzisha mfuko maalum wa fedha, halitosaidia cho chote. Kinachohitajiwa ni mageuzi katika mfumo wa taasisi za benki ili kuzuia mzozo wa aina hiyo kutokea mara nyingine tena, na sio kudai fedha ili kujiandaa kukabiliana na madhara yake."

" Bado ipo hatari kuwa hatimae ni walipa kodi ndio watakaolazimika kuubeba mzigo huo kwa sababu mfuko wa fedha hautotosha," linasema gazeti la "BADISCHE ZEITUNG" na kuongezea:

"Muhimu zaidi ni kuwepo kanuni na masharti dhahiri au hata kupiga marufuku kabisa biashara hatari katika masoko ya fedha. Barabarani kuna viwango vya mwendo, lakini  benki na washawishi wake hawakuwekewa mipaka yo yote."

Kwa maoni ya gazeti la "AUGSBURGER ALLGEMEINE" hata mfuko wa fedha wenye kiasi cha Euro bilioni 40 au bilioni 50 hautosaidia ikiwa benki kama vile Hypo Real Estate au Commerzbank zimeshaanza kuyumbayumba. Likiendelea linaandika:

"Kwa hivyo, ni muhimu kabisa kuhakikishwa tangu mwanzoni kuwa fedha zitakazowekwa katika mfuko huo maalum, zitatosha kukabiliana na matatizo iwapo yatatokeza."

Tukipindukia mada nyingine, gazeti la "BERLINER ZEITUNG" linasema, "Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na Waziri Mkuu wake Francois Fillon wameahidi kuwa wameuelewa ujumbe wa wapiga kura na watachukua hatua zinazohitajika." Likiendelea linaandika:

"Lakini ukweli ni kuwa si Sarkozy wala Fillon wanaoweza kutimiza matakwa ya wapiga kura- nafasi zaidi za ajira; nyongeza ya mishahara; kupunguziwa kodi ya pato - kwani mzozo wa fedha umeacha madhara yake. Kwa hivyo serikali haina budi kufanya mageuzi yatakayoumiza ili iweze kutekeleza mahitaji ya hivi sasa na kuendelea kulipia huduma za kijamii. Hata ikiwa Sarkozy ameifanyia marekebisho madogo serikali yake, kuonyesha mageuzi, ukweli unasalia pale pale, yaani hakuna kitakachobadilika."

Mwandishi:Martin,Prema/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman