Syria yavunja mzingiro wa waasi
8 Januari 2018Jeshi la Syria limevunja mzingiro uliokuwa umewekwa na waasi kuizunguka kambi yake Mashariki mwa mji mkuu Damascus, na kuwakomboa wanajeshi wapatao 200. Wakati huo huo vikosi vitiifu kwa Rais wa Syria Bashar al-Assad vinasonga mbele kuingia katika ngome za mwisho za waasi katika mkoa wa Idlib unaopakana na Uturuki.
Wanajeshi wa kikosi maalumu cha jeshi la serikali wameingia katika kambi hiyo iliyo kwenye kwenye eneo la Ghouta Mashariki, wakisaidiwa na ndege za kivita za Urusi. Waasi wa kundi lenye Itikadi kali za Kiislamu la Ahrar al-Sham waliizingira kambi hiyo mwezi Novemba mwaka jana katika juhudi za kupunguza shinikizo la serikali dhidi ya miji na vijiji vya Ghouta Mashariki vilivyokuwa chini ya udhibiti. Kukombolewa kwa mji huo kumetangazwa na kituo cha televisheni cha al-Ikhbariya kinachomilikiwa na serikali ya mjini Damascus, pamoja na shirika linalofuatilia vita vya Syria.
Kuvunjwa kwa mzingiro huo ni mojawapo ya mfululizo wa mafanikio vinayoyapata vikosi vitiifu kwa serikali ya Syria mnamo wiki za hivi karibuni. Hapo jana vikosi hivyo viliukamata pia mji wa Sinjar, ambao ni kiunganishi muhimu cha miji miwili mikubwa zaidi nchini Syria, Damascus na Aleppo.
Hali hii mpya imewalazimisha maelfu ya raia kukimbia wakielekea Kaskazini mwa mpaka na Uturuki, huku wakitaabika katika msimu wa baridi kali. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa watu takribani milioni 2.6 wanaishi katika mkoa wa Idlib, wakiwemo zaidi ya milioni 1.1 walikwenda huko wakikimbia mapigano katika sehemu nyingine za Syria.
Mashambulizi ya serikali katika mkoa wa Idlib ambao una ngome za makundi ya waasi yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida yalitarajiwa baada ya kushindwa kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu- IS mwishoni mwa mwaka uliopita. Wiki jana, Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema operesheni dhidi ya IS imemalizika, na hiyo iliashiria kuwa sasa ni zamu ya wanamgambo wenye uhusiano na al-Qaida.
Haijulikana mashambulizi ya sasa mkoani Idlib yanaazimia kufikia malengo gani, lakini inafahamika kuwa kujaribu kuukomboa mkoa mzima kwaweza kuchukua muda mrefu na kusababisha umwagaji mkubwa wa damu. Duru za waasi zinakadiria kuwa inachokilenga serikali kwa sasa ni kuikamata kambi ya waasi ya Abu Zuhour iliyo kwenye ncha ya kusini ya mkoa wa Idlib, na kuisalimisha njia muhimu inayounganisha miji ya Damascus na Aleppo.
Uturuki ambayo inawaunga mkono waasi, imepeleka waangalizi wa kijeshi katika mkoa wa Idlib, ikiwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa kati yake, Iran na Urusi kwa madhumuni ya kupunguza mivutano.
Mwanaharakati mmoja wa upinzani ambaye hakupenda jina lake litajwe, amesema waasi wanajikuta katika wakati mgumu, wakikabiliwa upande mmoja na vikosi vya serikali, na upande mwingine mbinyo wa masalia ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu.
Huku hayo yakiarifiwa, kundi linalochunguza haki za binadamu nchini Syria limesema kuwa mripuko uliotokea katika makao makuu ya kundi ogo la waasi mkoani Idlib umeuwa watu 23 na kujeruhi wengine wengi, miongoni mwa wahanga wakiwemo raia.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga