Syria yatumia jeshi kuwavunja nguvu wapenda mageuzi
25 Aprili 2011Maelfu ya wanajeshi wa Syria, wakisaidiwa na vifaru, wamepelekwa Daraa kuwavunja nguvu wapinzani katika mji huo, wanaolalamika dhidi ya utawala wa miaka 11 wa rais Bashar al Assad. Hii ni mara ya kwanza kwa vifaru kupelekwa katika eneo wanakoishi raia. Kwa mujibu wa wanaharakati, watu wasiopungua 25 wameuwawa hadi sasa katika mji huo.
Mashahidi wameliambia shirika la habari la Reuters wameona miili barabarani karibu na msikiti, baada ya wanajeshi hao kuingia mjini humo.
Hakuna uwezekano wa kupata habari za kuaminika kuhusu idadi ya waliouwawa. Syria imewapiga marufuku waandishi wa habari wa kigeni kuingia nchini humo. Mawasiliano ya simu na umeme yamekatwa mjini Daraa. Hata hivyo, baadhi ya watu wenye simu za mikono wameweza kuwasiliana na jamaa na marafiki zao.
"Hasara ni kubwa na magari ya kusafirisha wagonjwa yanapata shida kutokana na mizinga inayofyetuliwa" amesema dereva mmoja aliyehojiwa kwa simu na shirika la habari la Ujerumani-DPA.
Wanaharakati wa haki za binaadam wamesema askari kanzu wanawaingilia na kuwakamata wapenda demokrasia. Wengi wamekamatwa Damascus na Homs.
Mtaalam wa masuala ya Mashariki ya kati, Lamis Andoni, anahofia utawala wa Syria hauko tayari kuridhia madai ya wapenda mageuzi..
"Matumizi ya nguvu yatazidi kuongezeka. Ninahofia hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Serikali haijajifunza-inataka kung'ang'ania kwa nguvu madaraka.Watazidi kuwakandamiza wamepanda mageuzi. Tunaweza kushuhudia damu zaidi ikimwagika."
Watu wasiopungua 350 wameuliwa tangu machafuko yaliporipuka Daraa, mji wa kusini unaopakana na Jordan. Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Jordan, Syria imeufunga mpaka wake na nchi hiyo ya kifalme.
Mkuu wa shirika linalopigania haki za binaadam la Umoja wa mataifa, Navi Pillay, ametoa mwito matumizi ya nguvu yakome haraka nchini Syria. Amesema ni jukumu la serikali kuwalinda raia na kuruhusu maendeleo ya amani.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,Afp,Dpa.
Mhariri: Miraji Othman