1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yasitisha mapigano

27 Februari 2018

Mwito wa kusitishwa mapigano kwa masaa matano uliotolewa na Urusi, katika eneo linalokaliwa na waasi nchini Syria la Ghouta Mashariki, karibu na Damascus, ili kuruhusu raia kuondoka kwenye eneo hilo umeanza kutekelezwa.

https://p.dw.com/p/2tOPT
Syrien Luftangriffe auf Ost-Ghuta
Picha: picture-alliance/Photoshot

Mwito wa kusitishwa  mapigano kwa masaa matano uliotolewa na Urusi hapo jana, katika eneo linalodhibitwa na waasi nchini Syria la Ghouta Mashariki, karibu na Damascus, ili kuruhusu raia kuondoka kwenye eneo hilo, linalolengwa na mashambulizi yanayofanywa na serikali inayoungwa mkono na Urusi, umeanza kutekelezwa. Hata hivyo imeelezwa kuwa hakukua na dalili zozote za haraka za kuandaliwa kwa njia itakayotumiwa na raia hao kupita, wakati wakiondoka kwenye eneo hilo.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin aliagiza usitishwaji mapigano wa kila siku kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana, na kuandaliwa kwa njia itakayotumika kwa ajili ya raia kupita, katika eneo hilo ambalo mashambulizi yanayofanywa na serikali yamesababisha vifo vya mamia ya raia tangu Februari 18. 

Shirika linaloangazia haki za binaadamu la nchini humo limesema kumekuwepo na hali ya utulivu mashariki mwa Ghouta tangu usiku wa jana, ingawa kulirushwa maroketi manne kwenye mji wa Douma majira ya asubuhi. Kulingana na shirika hilo, watu 550 wameuawa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na serikali ya Syria kwa kushirikiana na Urusi.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema hapo jana kwamba kufikiwa hatua hiyo, kulifuatia makubaliano na vikosi vya Syria, kwa lengo la kuwasaidia raia kuondoka na kuwahamisha wagonjwa na majeruhi. 

Russland Präsident Putin beim russischen Präsidentenrat
Rais wa Urusi Vladimir Putin aliyetoa mwito wa kusimamishwa mapigano Syria ili kuruhusu misaada ya kiutuPicha: picture alliance/TASS/dpa/V. Prokofyev

Lakini, msemaji wa moja ya makundi makuu ya waasi katika eneo hilo la Ghouta Mashariki la Failaq al-Rahman, ameituhumu Urusi kwa kuwasilisha hoja ya kuwahamisha raia kinguvu ama kuendelea kuuawa kwa mashambulizi, na kuiita hatua hiyo kama "uhalifu wa Urusi".

Baadhi wadhihaki agizo hilo la Putin.

Hapo jana kwenye mkutano ulioikutanisha kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC mjini Geneva, msemaji wa kamati hiyo Iolanda Jaquement alisema kamati hiyo imeikaribisha taarifa hiyo njema ya rais Putin ya kutaka kusitishwa mapigano kila siku kwa siku tano mfululizo. Ingawa alionya kwamba upatikanaji wa misaada ya kiutu ni lazima utofautishwe na makubaliano ya kisiasa. Bi. Jaquement aidha, alisisitiza kwamba zoezi la kuwahamisha raia hao lizingatie utu na liwe la hiyari.

Baadhi ya raia waliopo kwenye eneo hilo linalokabiliwa na machafuko wamedhihaki agizo hilo la rais Putin la kusitishwa mapigano. Ingy Sedky, anayefanya kazi na shirika la kimataifa la msalaba mwekundu alisema, ili hatua hiyo iweze kutekelezeka, inahitaji mipango mizuri na kutekelezwa katika wakati ambapo kuna makubaliano miongoni mwa makundi yanayohasimiana.  

Katika hatua nyingine, shirika la habari la Urusi, TASS hii leo limearifui kwamba Urusi imewatuhumu waasi nchini Syria kwa kufanya mashambulzi kwenye njia zilizofunguliwa kwa ajili ya raia kupita kutoka mashariki mwa Ghouta. shirika hilo limesema, kutokana na mashambulizi hayo, hakuna raia hata mmoja ambaye ameweza kuondoka kupitia njia hizo.

Ghouta Mashariki ni ngome muhimu ya mwisho karibu na Damascus, kwa waasi wanaopambana ili kumuondoa madarakani rais Bashar al Assad, ambaye tayari amewafurusha waasi kutoka kwenye maeneo mengi, huku akiungwa mkono kijeshi na Urusi na Iran. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha siku ya Jumamosi azimio la kutaka siku 30 za usitishwaji wa mapigano nchini humo.  

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/dpae.
Mhariri:Yusuf Saumu