Syria yashutumiwa kutumia gesi ya sumu
17 Machi 2015Katika ripoti yake iliyotolewa leo, Amnesty International imesema imekuwa ikifuatilia mfululizo wa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la serikali ya Syria kati ya tarehe 11 na 29 za mwezi Novemba mwaka jana, ambayo limesema yaliuwa raia 115 katika mji wa Raqqa Kaskazini mwa Syria.
Mji huo ulitumiwa kama makao makuu ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS, tangu lilipotangaza utawala wake katika maeneo liliyoyateka. Mnamo tarehe 25 Novemba pekee, watu 60 waliuawa katika mashambulizi ya aina hiyo, limesema Amnesty International katika ripoti yake.
Umoja wa Mataifa nao waja juu
Huku hayo yakiarifiwa, wachunguzi wa uhalifu wa kivita wa Umoja wa Mataifa wamesema hii leo mjini Geneva, kwamba wako tayari kukabidhi orodha yake ya siri ya washukiwa kwa chombo chochote kinachoweza kufungua kesi dhidi yao.
''Kwa wakati huu tunaweza kusaidia vyema mchakato wa kutaka haki ifanyike. Tutatoa majina na taarifa kuhusu washukiwa wa uhalifu huo kwa waendeshamashita wa nchi ambao wako tayari kuifikisha kesi hiyo katika mahakama yenye uwezo wa kuisikiliza, na ambayo haiegemei upande wowote'', amesema Paulo Pinheiro, mwenyekiti wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa.
Mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililowasilishwa na Marekani, ambalo liliilaani Syria kwa kutumia gesi ya Klorini, na kutishia kuchukua hatua dhidi ya nchi hiyo ikiwa itatumia tena gesi hiyo katika mapigano.
Gesi ya Klorini ilitumika
Wakati huo huo shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria ambalo lina makao yake nchini Uingereza limesema kwamba Syria ilifanya shambulio la kutumia gesi ya sumu, ambalo liliuwa watu wasiopungua sita katika kijiji cha Salmin kilichoko mkoani Idlib. Limesema wahanga hao ni pamoja na watano kutoka familia moja, yaani baba, mama na watoto wao watatu.
Kama ushahidi kwa madai yake, shirika hilo, The Syria Observatory for Human Rights, limetumia taarifa za kitabibu ambazo zimesema watu hao walikufa kutokana na gesi iliyotoka ndani ya mabomu yaliyo mithili ya mapipa, likiongeza kuwa gesi hiyo ni aina ya Klorini.
Wauguzi waliweka mtandaoni mkanda wa video ambao uliwaonyesha watoto wanaopata taabu kupumua. Kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binadamu, watu wengine zaidi ya 20 walijeruhiwa katika shambulio hilo, ambalo hata hivyo, shirika la habari la Reuters lililoripoti taarifa hii halikuweza kuthibitisha.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/ape/afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman