1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yakabidhi asilimia 65 ya silaha za kemikali

15 Aprili 2014

Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Silaha za Atomiki, OPCW, wamesema wanatiwa wasiwasi na kasi ya Syria katika kukabidhi silaha zake za atomiki.

https://p.dw.com/p/1Bi3Y
Meli ya Dernmark inayopakia shehena ya silaha za kemikali za Syria
Meli ya Dernmark inayopakia shehena ya silaha za kemikali za SyriaPicha: Reuters

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Silaha za Atomiki, OPCW, shehena ya 13 ya silaha za kemikali za Syria ilipakiwa kwenye meli kwenye bandari ya Latakia jana, na kutimiza asilimia 65 tu ya shehena iliyotangazwa ambayo imeondolewa ndani ya Syria. Mkurugenzi mkuu wa OPCW Ahmet Uzumcu amesema hatua hiyo ya jana ilikuwa muhimu na ya lazima, na kuongeza lakini kwamba angependa kuona juhudi zaidi zikifanyika.

Uzumcu amesema kiwango cha silaha zinazokabidhiwa, na pia kasi ya kukabidhi silaha hizo vinapaswa kuongezeka sana, ili Syria iweze kwenda sambamba na muda uliopangwa kukamilisha mchakato huo ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu.

Muda wazidi kuyoyoma

Na katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema anatambua kuwa Syria haikuweza kuheshimu muda wa mwisho uliokuwa umewekwa mwanzoni, ambao ulikuwa tarehe 13 April, kuwa imeondoa silaha zote zilizo mahali inakoweza kufika, na kuonya kwamba muda mpya uliowekwa ulikuwa ukikaribia.

Watu zaidi ya elfu moja walidaiwa kuuwa kwa silaha za sumu za Syria mwaka uliopita
Watu zaidi ya elfu moja walidaiwa kuuwa kwa silaha za sumu za Syria mwaka uliopitaPicha: Reuters

Dujarric amesema kutohishimu ratiba ya tarehe 27 Aprili kunaweza kuwa na athari mbaya kwenye azma ya kukamilisha zoezi hilo tarehe 30 Juni.

Mapema mwezi huu serikali ya Syria ilianzisha tena zoezi la kukabidhi silaha zake za kemikali, baada ya kulisimamisha kwa muda kutokana na kile ilichokiezea kuwa sababu za kiusalama.

Afisa anayeratibu shughuli za ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na OPCW nchini Syria Sigrid Kaag aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili kuwa bado Syria inao uwezo wa kumaliza kazi ya kukabidhi silaha zake za kemikali kwa muda uliopangwa.

Dernmark na Norway zatoa usafiri

Meli za Norway na za Denmark zinashiriki katika shughuli ya kupakia silaha hizo za kemikali za Syria kutoka bandari ya Latakia magharibi mwa Syria. Shehena ya hatari zaidi kutoka Syria itachukuliwa na meli ya jeshi la Marekani ambayo inayo mitambo yenye uwezo wa kuiangamiza.

Umoja wa Mataifa unasema muda wa zoezi la kukabidhi silaha unakwisha haraka
Umoja wa Mataifa unasema muda wa zoezi la kukabidhi silaha unakwisha harakaPicha: LOUAI BESHARA/AFP/Getty Images

Wakati huo huo taarifa za hivi karibuni kutoka Syria zinaeleza kuwa mashambulizi dhidi ya mji mkuu Damascus yamemuuwa mtoto mmoja na kujeruhi watu wengine zaidi ya 40. Shirika la habari la nchi hiyo, SANA limemnukuu afisa wa polisi akisema mashambulizi hayo yalifanywa na waasi dhid shule iliyoko katika mtaa wa Bab Touma mjini Damascus.

Waasi bado wanayadhibiti maeneo kadhaa kandoni mwa mji huo, ambaya wanayatumia kuushambulia mji mkuuu huo mara kwa mara. Mashambulizi yao mengi hulenga mitaa ya watu matajiri wanakokaa mabalozi wa nchi za nje, pamoja na eneo kongwe la mji huo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri: Ssessanga