1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yajiunga na makubaliano ya mazingira ya Paris

Caro Robi
8 Novemba 2017

Syria imeuambia mkutano wa kimataifa wa mazingira unaoendelea Bonn, Ujerumani kuwa itajiunga na makubaliano ya Paris hivyo kuiacha Marekani kuwa nchi pekee duniani iliyo nje ya makubaliano hayo ya kuyalinda mazingira.

https://p.dw.com/p/2nFin
COP23 UN Klimakonferenz in Bonn Eröffnung
Picha: Getty Images/AFP/P. Stollarz

Msemaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa Nick Nutfall amesema serikali ya Syria imetangaza jana Jumanne kuwa ina nia ya kujiunga na makubaliano ya Paris baada ya mjumbe wa Syria Wadah Katmawi ambaye ni naibu waziri wa serikali za mitaa na mazingira kukiambia kikao cha mazungumzo ya COP23 kuwa nchi yake imeamua kujiunga na makubaliano hayo.

Marekani ilikuwa miongoni mwa nchi 195 zilizotia saini makubaliano hayo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi mwaka 2015, lakini Rais wa nchi hiyo Donald Trump mnamo mwezi Juni mwaka huu alitangaza kuwa nchi yake inajiondoa kutoka makubaliano hayo kwa hoja kuwa hayatilii maanani maslahi ya Marekani.

Syria sasa itahitaji kuwasilisha rasmi ombi lao la kujiunga na makubaliano hayo kwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini New York kabla haijatangazwa rasmi kuwa imeyaidhinisha makubaliano ya Paris.

Marekani ni nchi pekee nje ya makubaliano ya Paris

Kulingana na mtandao wa bunge la Syria, mswada ulipitishwa tarehe 22 mwezi Okotoba kuidhinisha nchi hiyo kujiunga na makubaliano hayo, kuambatana na katiba ya nchi hiyo ambayo inawianisha kulindwa kwa mazingira.

COP23 UN Klimakonferenz in Bonn Eröffnung  Patricia Espinosa
Patricia Espinosa Katibu mtendaji wa mkataba wa mazingira wa Umoja wa MataifaPicha: Reuters/W. Rattay

Wajumbe wanaohudhuria mkutano huo wa mazingira ambao leo umeingia siku yake ya tatu wameipongeza hatua hiyo ya Syria ambayo ni nchi ya 197 kujiunga na makubaliano hayo ya kuyalinda mazingira yanayolenga kupunguza viwango vya joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Rais Trump sio miongoni mwa viongozi wa dunia walioalikwa katika mkutano wa kilele wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi utakaofanyika Paris mwezi ujao. Nchi 100 ambazo ziko katika mstari wa mbele kutekeleza makubaliano ya Paris ndizo zilizoalikwa katika mkutano huo unaokuja baada ya huu wa Bonn.

Wakati huo huo, kundi la kampuni kubwa za Ujerumani zimeitaka Serikali kusitisha uzalishaji wa umeme utokanao na makaa ya mawe na kuimarisha teknolojia za kisasa katika shughuli za kiviwanda.

Kampuni hizo zikiwemo za simu na mawasiliano Siemens, SAP na Deutsche Telekom zinazojiita wakfu wa nyuzi mbili zimetoa wito wa kuwepo njia madhubuti ya kuondokana kutoka matumizi ya nishati ya makaa ya mawe ambayo inachangia asilimia 40 ya umeme Ujerumani.

Wakfu huo wa nyuzi mbili unaozijumuisha kampuni kubwa Ujerumani ulioanzishwa miaka 10 iliyopita unajichukulia kuwa jukwaa la kusuluhisha matatizo ya kimazingira yanayoiukumba Ujerumani na imeitaka Serikali kulenga kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani hadi asilimia 95 ifikapo mwaka 2050.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri:Josephat Charo