1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yaishutumu Israel kwa mashambulizi

13 Januari 2017

Jeshi la Syria limesema kuwa Israel ilirusha makombora katika uwanja wa kijeshi nje ya Damascus. Kituo cha habari cha serikali kimesema makombora manane yalirushwa usiku wa kuamkia leo na kulipuka katika uwanja huo.

https://p.dw.com/p/2VkUG
Syrien Damaskus Stadtansicht
Picha: picture alliance/AP Photo/H. Ammar

Uwanja huo wa ndege hutumika zaidi na kikosi maalumu cha walinzi na awali ulitumika kama kituo cha kurusha makombora kuelekea ngome zilizokuwa za waasi karibu na Damascus wakati wa vita nchini Syria. Uwanja huo Kusini Magharibi mwa Damascus. Kulingana na taarifa kutoka kwa Jesh hilo, haijabainika iwapo kulikuwa na majeruhi wowote japo mashambulizi hayo yalisababisha kuzuka kwa moto. 

Jeshi la Serikali ya Syria laionya Israel

Jeshi hilo la serikali ya Syria lilisema kuwa hatua zitachukuliwa kutokana na tukio hilo. Katika taarifa, jeshi hilo lilisema  kuwa linaionya Israel kuhusu hatua kali zitakozochukuliwa na kusisitiza kuwa litaendelea na vita dhidi ya ugaidi na kukabiliana na wavunjaji sheria.
Lakini kulingana na shirika la habari la AFP; jeshi la Israel halikusema lolote kuhusiana na ripoti hiyo ijapokuwa hivi karibuni, waziri wa ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman alisisitiza msimamo wa serikali yake wa kutoingia katika vita na Syria. Awali Israel ililenga kundi la Hezbollah kutoka Lebanon ambalo linapigana bega kwa bega na jeshi la Syria. 
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umezionya pande zote mbili dhidi ya kuifanya hali kuwa mbaya zaidi kwakuwa kuna mkataba wa kusitisha mapigano kote nchini humo. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria , Staffan de Mistura, hapo jana alisema kuwa mktaba huo bado unazingatiwa japo kuna maeneo kidogo ambayo yamekiuka mkataba huo huku mashirika yanayofuatilia hali ilivyo yakiripoti kuweko kwa mashambulizi karibu na Damascus.
Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, lilisema kuwa jeshi la serikali ya Syria liliimarisha kampeini ya kulikomboa eneo la Wadi Barada liliko viungwani mwa Damascus dhidi ya uthibiti wa waasi. 
Shirika hilo liliripoti ongezeko la mashambulizi ya angani katika eneo hilo ambako huduma za ugavi wa maji yanayowatosheleza zaidi ya watu milioni 5 mjini Damascus zimekatizwa kutokana na kuzuka upya kwa ghasia .
De Mistura aliwaambia wanahabari huko Geneva kuwa vijiji vitano katika eneo la Wadi Barada viliafikia makubaliano na serikali lakini viwili vilishindwa kuafikia makubaliano hayo. 

Syrien Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Watu wengine wafariki katika shmabulizi la kujitolea mhanga 
Mbali na hayo, mlipuaji wa kujitoa mhanga hapo jana jioni aliwauwa takriban watu saba katika eneo hilo la Damascus lililoko chini ya ulinzi mkali hilo likiwa jambo nadra kutokea katika ngome za  jeshi la serikali ya nchi hiyo. 
Shambulizi hilo lilitokea katika wilaya ya Kafr Sousa, makazi ya mawaziri na maafisa wakuu wa usalama . Kulingana na shirika hilo la kufuatilia haki za binadamu, miongoni mwa waliofariki, wanne walikuwa wanajeshi. 
Balozi huyo wa Umoja wa Mataifa alionya kuwa  makundi hayo yaliojihami katika mkoa wa Idlib yalizuia mabasi 23 na madereva wa Syria kuondoka katika eneo hilo kupeleka msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa wa vita nchini humo. 


Mwandishi: Tatu Karema/dw.com/English
Mhariri: Iddi Ssessanga