1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yaanza mwaka kwa mapigano zaidi

MjahidA2 Januari 2013

Waasi nchini Syria hii leo wameongeza mashambulizi yao dhidi ya uwanja wa ndege unaodhibitiwa na jeshi la serikali, katika mkoa wa kaskazini wa Idlib

https://p.dw.com/p/17CCC
Waasi wa Syria
Waasi wa SyriaPicha: Reuters

Waasi hao walio na nia ya kuing'oa madarakani serikali ya Bashar Al Assad waliushambulia uwanja wa ndege wa Taftanaz, na kuzua mapigano makali kati yao na vikosi vya serikali. Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria lililo na makao yake mjini London, Uingereza, kumekuwa na majeruhi pande zote mbili ingawa halikutangaza wazi idadi kamili.

Kwa sasa waasi nchini Syria wanadhibiti miji kadhaa hasa katika eneo la kaskazini karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uturuki. Hata hivyo imekuwa vigumu kwa vyombo vya habari vya kimataifa kuthibitisha na kusimulia mambo yanavyoendelea nchini humo kufuatia serikali kupiga marufuku vyombo hivyo tangu kuanza kwa maadamano ya kutaka mageuzi ya kidemokrasia mwezi Machi mwaka wa 2011.

Mkuu wa baraza la kitaifa la Syria George Sabra
Mkuu wa baraza la kitaifa la Syria George SabraPicha: DW / Marx

Wakati huo huo, raia mmoja wa Australia, Abu al-Walid al-Australi, aliyeungana na waasi kupigana na vikosi vya serikali, ameuwawa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria, Rami Abdel Rahman, Abu al-Walid aliuwawa Disemba 30 katika eneo la Wadi Deif baada ya waasi kuanzisha mashambulizi kwa nia ya kuiteka ngome hiyo mnamo Desemba 28.

Serikali ya Australia imeuilaani vikali utawala wa Assad kwa kufanya mashambulizi dhidi ya raia wake. Serikali hiyo pia imewaondoa wanadiplomasia wa Syria nchini mwake na kumtaka Assad aondoke madarakani mara moja.

Moshi unaotokana na mashambulizi Syria
Moshi unaotokana na mashambulizi SyriaPicha: picture-alliance/dpa

George Sabra rais kundi la upinzani la Baraza la kitaifa la Syria amesema anatumai mapinduzi yao yataendelea kwa njia ilio sawa na kuwa watapata ushindi. "Natumai jamii ya Kimazaifa itatambua kile kinachoendelea Syria, na kutekeleza wajibu wao wa kutoa msaada wa kibinaadamu na kuwasaidia wasyria kujilinda kwa kuwapa silaha ili kuwapa uhuru watu wa Syria katika kutafuta amani na hadhi yao" Alisema George Sabra

Waasi nchini Syria wanajumuisha majeshi yaliyoasi, raia walio na silaha, na wapiganaji wa kimataifa wakiwemo makundi kadhaa ya kiislamu. Tangu kuanza kwa ghasia nchini humo zaidi ya miezi 20 iliyopita watu zaidi ya 46,000 wameuwawa huku wengine wengi wakiachwa bila makao.

Mashambulizi zaidi

Siku ya Mwaka mpya raia nchini humo waliuanza mwaka kwa mashambulizi makali karibu na mji wa Damascus na pia kufungwa kwa uwanja wa ndege wa mji wa Allepo.

Wanajeshi waliotiifu kwa Bashar Al Assad
Wanajeshi waliotiifu kwa Bashar Al AssadPicha: Reuters

Tukio hilo lililosababisha mauaji ya watu 69 limetilia shaka uwezekano wa kuwepo amani na kuumaliza mgogoro wa Syria. Video iliyotumwa katika mtandao na waasi inaonesha wanajeshi wa serikali wakiwadunga visu na kuwaua wafungwa wawili. Huku hayo yakiarifiwa mwanadiplomasia wa Uturuki amesema wanajeshi 20 wa Syria wameasi hapo jana na kukimbilia nchini humo.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri: Josephat Charo