Syria yaanza kusafirisha silaha za sumu
8 Januari 2014Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na udhibiti wa silaha za sumu OPCW limesema shehena ya mwanzo ya silaha hizo zilizowasilishwa katika bandari ya Latakia, zimepakiwa katika meli ya Denmark ambapo kwa hivi sasa inaelekea katika bahari ya kimataiafa.
Syria ilikubali kuangamiza silaha zake za sumu mpaka ifikapo mwezi Juni mwaka huu, chini ya mpango uliopendekezwa na Urusi na kukubaliwa na Marekani baada ya kutokea shambulio la sumu aina ya Sarin la Agosti 21, ambalo mataifa ya magharibi yanalaumu upande wa majeshi la rais Bashar al Assad. Na serikali ya Damascus inalalamikia waasi kuhusika na mkasa huo wa mauwaji.
Sababu za kuchelewa safari
Vita, hali mbaya ya hewa, ukiritimba na matatizo ya kiufundi ni miongoni mwa sababu zilizochangia kutotimizwa hatua ya kuondosha shehena hiyo ya silaha za sumu kutoka Syria katika muda uliopangwa wa Desemba 31.
Shirika OPCW, halijataja asilimia ngapi za kiwango cha silaha hizo za Syria kimeondolewa nchini humo kunakokadiriwa kuwepo kiasi cha tani 1,300 na kwamba katika meli hii ya Denmark kumebeba makontena manane. Taarifa zinasema kuwa meli hiyo imesindikizwa na vikosi vya jeshi la wanamaji la mataifa ya Denmark na Norway.
Maamuzi ya upinzani kuhusu mkutano wa amani
Katika duru nyingine upinzani unaungwa mkono na matiafa ya magharibi imeahirisha kutoa uamuzi kama utashiriki kufanya mazungumzo ya amani na rais Assad kwa shabaha ya kumaliza mapigano yaliodumu kwa karibu miaka mitatu nchini humo.
Taarifa ya upande huo ambao unaishi uhamishoni umesema umauzi wa kushiriki ama kutoshirika utatolewa wiki ijayo.
Muungano huo wa upinzani wa kitaifa unakabiliwa na shinikizo kutoka kwa matiafa ya magharibi la kushiriki mkutano wa amani wa Januari 22, ambao kwa hivi sasa unaonekana kama jitihada ya msingi katika kumaliza kabisa vitia vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.
Hata hivyo upande huo uliwahi kusema uko tayari kushiriki mkutano huo kwa masharti ya kiongozwa na lile la kuondoka madarakani kwa rais Assad, jambo ambalo limepingwa na serikali ya Syria.
Ama maseneta kutoka vyama vya Democratic na Republican nchini Marekani wametoa wito kwa taifa lao kuchukua zaidi idadi ya wakimbizi ambao wanakimbia makazi yao kutokana na vita vya Syria. Kiasi ya wakimbizi 31 kutoka Syria kati ya wakimbizi milioni 2.3 waliruhusiwa kuingia nchini Marekani kwa mwaka wa fedha uliomalizika Oktoba.
Hadi sasa kiasi ya wakimbizi 135,000 wameomba hifadhi nchini humo lakini sheria kali za uhamiaji zimefanya idadi hiyo kutofanikiwa kuingia. Hata hivyo Marekani imeahidi kutoa kiasi cha dola bilioni 1.3 kama msaada wa kiutu.
Mwandishi: Sudi Mnette RTR
Mhariri: Mohamed Khelef