1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria na Lebanon kuanzisha uhusiano wa kibalozi

P.Martin13 Agosti 2008

Rais wa Syria Bashar al-Assad aliushangaza ulimwengu alipotangaza Paris kuwa karibuni Syria itakuwa na majadiliano ya kuanzisha uhusiano wa kibalozi pamoja na Lebanon.

https://p.dw.com/p/EwDh

Siku hiyo ndio imewadia,kwani leo Rais wa Lebanon Michel Suleiman ameanza ziara ya siku mbili katika mji mkuu wa Syria Damascus.Uhusiano wa kibalozi huenda ukafungua njia ya kusawazisha uhusiano kati ya majirani hao wawili.

Ingawa Lebanon ni taifa huru tangu mwaka 1943 na Syria nayo ilipata uhuru wake mwaka 1946,majirani hao wawili hadi hii leo hawakubadilishana mabalozi.Yaonekana kana kwamba uhusiano wa nchi hizo mbili ni uhusiano wa kihistoria wa kutegemeana.

Hadi hivi sasa Wasyria wengi hawaitazami Lebanon kama ni taifa huru,bali kama jimbo la 19 na hivyo ni sehemu ya Syria.Hiyo inatokana na historia ya eneo hilo.Kwani hadi Vita Vikuu vya Kwanza zote mbili zilikuwa sehemu ya Milki ya Utawala wa Kifalme wa Ottoman,iliyoanzia Ufalme Cyprus kuenea hadi Iraq ya leo na kufikia Palestina.

Wakati wa Vita Vikuu vya mwanzo Uingereza na Ufaransa zilikubaliana kugawana maeneo hayo.Syria na Lebanon zikawa chini ya uongozi wa Ufaransa.Na katika mwaka 1920 utawala wa Kifaransa uliokuwa na makao yake mjini Damascus ulizindua taifa dogo la Lebanon ambako wengi walikuwa Wakristo wa madhehebu ya Kimaronite.Taifa hilo katika mwaka 1926 likawa Jamhuri ya Lebanon iliyojiamulia kwa hiyari kubakia chini ya mamlaka ya Ufaransa na ilipewa uhuru wake mwaka 1943.Lakini hadi hii leo hasa Wakristo wa Lebanon wanaelemea zaidi upande wa Ufaransa na nchi za magharibi,wakati Waislamu wakielekea nchi za Kiarabu na hasa Syria,iliyopata uhuru wake mwaka 1946 baada ya kumalizika Vita Vikuu vya Pili.

Kwa sababu ya matokeo hayo ya kihistoria,Damascus haikusita kuitazama Lebanon kama ni sehemu ya eneo la asili.Na Syria kwa miongo mingi imetumia ushawishi wake wa kisiasa na kijeshi katika nchi jirani. Hasa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon kuanzia 1975 hadi 1990,Syria iliyatumia makundi ya makabila na dini tofauti kendeleza maslahi yake.

Muda mfupi tu baada ya vita hivyo kuanza,Syria ilipeleka vikosi vyake nchini Lebanon,kurejesha amani na utulivu.Lakini ikadhihirika kuwa hiyo ilikuwa kama njia ya kuidhibiti Lebanon.Vikosi hivyo viliendelea kubakia huko hata baada ya vita hivyo kumalizika rasmi kuambatana na Makubaliano ya Taif.

Majeshi hayo yaliondoka Lebanon mwaka 2005,kufuatia maandamano makubwa yaliyofanywa dhidi ya Syria baada ya waziri mkuu wa wakati huo Rafik Hariri kuuawa katika shambulizi la bomu.Syria ikalaumiwa kuhusika na mauaji hayo.Hadi hii leo Damascus inakanusha kuhusika na mauaji hayo na hata ya viongozi wengi wengine baadae.Syria ambayo haikutaka ikijikuta imetengwa,iliinyoshea Beirut mkono wa urafiki, lakini iliendelea kudumisha uhusiano wake na Hezbollah.Kusawazishwa kwa uhusiano kati ya Beirut na Damascus kumesaidia pia kwa sehemu fulani kuumaliza mgogoro kati ya serikali ya Waziri Mkuu Fouad Siniora na Hezbollah nchini Lebanon.

Ziara inayofanywa leo na Rais wa Lebaon mji mkuu wa Syria Damascus,inatazamwa kwa mashaka na wachambuzi wa kisiasa.Hawaamini kuwa Syria itabadilisha hivyo msimamo wake.Kwa hivyo wanaonya kuwa taarifa za kisiasa zitakazotolewa zisichukuliwe kama ushahidi wa kufanikiwa au kushindwa ziara hiyo.Cha muhimu zaidi ni kile kitakachofuatia baada ya ziara hiyo kumalizika.