1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Mashambulizi ya serikali yauwa watu 98 Ghouta

20 Februari 2018

Jeshi la Syria limefanya mashambulizi makali dhidi ya eneo la Ghouta Mashariki linalodhibitiwa na waasi, na duru za wanaharakati zimeeleza kuwa watu wasiopungua 98 wameuawa katika mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/2syOZ
Syrien Luftangriffe gegen Ost-Ghouta
Ghouta Mashariki baada ya mashambulizi ya serikaliPicha: Getty Images/AFP/H. Al-Ajweh

Mashambulizi ya anga ya jeshi la Syria dhidi ya ngome za waasi katika viunga vya Ghouta Mashariki yalianza usiku wa kuamkia leo, na taarifa za hivi punde zimeeleza kuwa hadi sasa yanaendelea. Kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, watu zaidi ya 100 wamekwishauawa katika mashambulizi hayo, wakiwemo watoto 20 na wanawake 15. Kulinga na shirika hilo, watu wengi bado wako chini ya kifusi cha nyumba zilizoharibiwa.

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusimamisha mara moja kwa mapigano hayo.

Urusi ambayo ni mshirika muhimu zaidi wa serikali ya Syria, imekuwa ikijaribu kuanzisha juhudi za kidiplomasia kupunguza uhasama, na kupigia debe kuanzishwa kwa maeneo salama mnamo wakati huu mapigano yanapozidi kupamba moto.

Urusi yashuku mpango wa siri

MSC 2018 Sergei Lawrow
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Reuters/R. Orlowski

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, amesema kinachokwamisha juhudi hizo ni kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kukataa kulitaka kundi la Jabhat al-Nusra, mojawapo ya makundi ya waasi katika eneo hilo nalo pia kusitisha mapigano.

''Miito yote hii ya kulitaka jeshi la Syria lisitishe mapigano, inaambatana na kukataa kutoa hakikisho kwamba kundi la Jabhat al-Nusra pia litaacha kupigana'', amesema Lavrov, na kuongeza kuwa inavyoelekea, miito hii ni njama za siri za kupunguza shinikizo dhidi ya Jabhat al-Nusra. 

Jabhat al-Nusra ina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida, na yenyewe inachukuliwa kimataifa kama kundi la kigaidi. Makundi mengine ya upinzani katika eneo Ghouta Mashariki, yanasema Serikali na mshirika wake Urusi wanatumia kisingizio cha kuwepo Jabhat al-Nusra kuendeleza kampeni yao ya mashambulizi ya anga.

Juhudi za kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe

Syrien Präsident Assad - Rede vor Diplomaten in Damaskus
Rais wa Syria, Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Presidency

Eneo la Ghouta Mashariki ni ngome ya mwisho ya waasi karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus. Mashambulizi katika sehemu hiyo ni mwendelezo wa operesheni zinazofanywa na jeshi tiifu ka rais Bashar al-Assad katika maeneo mengi ya nchi, katika juhudi za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimekuwa vikiendelea nchini humo kwa miaka saba sasa. 

Hata hivyo, mashambulizi haya mapya yametajwa kuwa makali zaidi, na ndio yameangamiza idadi kubwa zaidi ya watu kwa muda wa miaka mitatu iliyopita. Wapinzani na wanaharakati wamearifu kuwa serikali imepeleka vikosi vya ziada kwa lengo la kuwafurusha waasi katika eneo hilo la Ghouta Mashariki.

Hakuna fununu ya jeshi la Syria kwenda Afrin

Syrien Manbij US-Truppen
Afrin imekuwa katika kilengeo cha Uturuki tangu mwanzoni mwa FebruariPicha: picture-alliance/AP Photo/S. George

Wakati huo huo, Uturuki imesema hadi wakati huu jeshi la serikali ya Syria halijaingia katika eneo la Wakurdi la Afrin kama ilivyokuwa ikitarajiwa kuanzia jana, na haijulikana iwapo linayo azma ya kufanya hivyo. Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesisitiza katika mazungumzo na kituo kimoja cha televisheni, kuwa Uturuki ambayo imepeleka wanajeshi wake kupambana na wanamgambo wa Kikurdi huko Afrin, halitasita kukabiliana na vikosi vya serikali ya mjini Damascus, iwapo vitapelekwa huko.

Wapiganaji wa kundi hilo la wakurdi linalopigwa vita na Uturuki, YPG, limeishutumu Urusi kuweka vizuizi katika mkataba uliokuwa umeripotiwa kati ya wapiganaji hao na serikali ya Syria, ambao ungeliruhusu jeshi kuingia katika eneo hilo lililo Kaskazini mwa nchi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, dpae, ape

Mhariri: Mohammed Khelef