Syria itatumia silaha za sumu ikishambuliwa
23 Julai 2012Wakati huo huo majeshi ya serikali yamekuwa yakipambana na waasi katika maeneo mbali mbali ya mji wa Damascus na Aleppo.
Onyo hilo lililotolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni, Jihad Makdissi, linakuja huku jumuiya ya kimataifa ikiingiwa na wasi wasi mkubwa kuwa Syria inajitayarisha kutumia silaha za sumu katika azma ya kukandamiza uasi uliodumu sasa miezi 16 dhidi ya rais Bashar al-Assad.
Syria haitatumia silaha za sumu ama silaha nyinginezo zisizo za kawaida dhidi ya raia wake, na itatumia tu silaha hizo iwapo itashambuliwa, Makdissi amewaambia waandishi habari mjini Damascus.
Hazina yoyote ya silaha za kemikali ambazo zipo, haitatumika kamwe dhidi ya Wasyria , amesema, na kuongeza kuwa lakini iwapo Syria itashambuliwa na mataifa ya nje, majenerali wataamua wakati gani na vipi watumie silaha hizo.
Matamshi hayo ya Makdissi yanakuja siku moja baada ya Marekani kusema kuwa afisa yeyote wa Syria atabeba jukumu iwapo atahusika katika kutoa ama kutumiwa kwa silaha za sumu.
Israel ina wasi wasi
Israel pia imesema jana kuwa ina wasiwasi juu ya silaha hizo za sumu kuwa huenda zikaingia mikononi mwa kundi la wanamgambo wa Kishia nchini Lebanon la Hezbollah.
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya kigeni amesema kuwa Syria inakataa kata kata madai ya jumuiya ya mataifa ya nchi za Kiarabu, Arab League- kuwa Assad ajiuzulu.
Mataifa ya Kiarabu yataka Assad ajiuzulu
Mkutano wa mjini Doha wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu umetoa taarifa ya wito kwa Assad kujitoa madarakani, akiahidiwa kuwa yeye pamoja na familia yake watapewa nafasi ya kutoka nchini humo kwa salama, kama alivyoeleza waziri mkuu wa Qatar, Hamad bin Jasim al Jaber al-Thani:
"Tunamuomba Bashar al-Assad ajiuzulu kwanza na atapewa njia salama ya kuondoka. Na pia tutatoa mchango wetu wa fedha kwa ajili ya wakimbizi , kiasi cha dola milioni 100, na pia tunazungumzia kuhusu ujumbe wa Kofi Annan ambao sasa utabadilishwa na kulenga zaidi kuwa wa kipindi cha mpito".
Vikwazo vyaimarishwa
Wakati huo huo ,Umoja wa Ulaya umeimarisha vikwazo vyake vya kukataza kutumwa silaha dhadi Syria na katika duru hii ya 17 ya vikwazo umoja huo umezuwia safari za ndege kwenda na kutoka nchini humo, na kuwaweka watu 12 katika orodha ya vikwazo hivyo.
Umoja wa Ulaya umeweka vikwazo vya silaha dhidi ya Syria Mei mwaka 2011, lakini imeimarisha vikwazo hivyo kwa kuzilazimisha nchi zote za umoja huo kukagua meli na ndege zinazokwenda nchini humo, na iwapo wanashuku kuwa shehena huenda ina silaha ama vifaa vitakavyotumika katika ukandamizaji nchini humo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae, afpe
Mhariri : Othman Miraji