SYDNEY: Cheney aendelea na ziara yake nchini Australia
23 Februari 2007Makamu wa rais wa Marekani, Dick Cheney, ameonya leo kwamba hatua ya China kujiimarisha kijeshi inaitia wasiwasi jumuiya ya kimataifa. Aidha Cheney amesema Marekani haiamini kirahisi kwamba Korea Kaskazini itatekeleza makubaliano yaliyofikiwa mjini Beijing kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Katika siku kamili ya kwanza ya ziara yake rasmi nchini Australia, Dick Cheney ametumia hotuba yake kwa kundi la Wamarekani na Waustralia mashuhuri kuwakanya wakosoaji wanaotaka Marekani na washirika wake waondoke nchini Afghanistan na Irak.
Ziara ya Dick Cheney mjini Sydney inalenga kuishukuru Australia kwa msaada wake nchini Irak katika vita dhidi ya ugaidi.
´Waziri mkuu Howard na taifa analolilitumikia hajayumbayumba katika vita dhidi ya ugaidi. Marekani inashukuru kwa hilo na dunia nzima inamheshimu.´
Machafuko baina ya polisi na waandamanji wanaoipinga ziara ya Dick Cheney yameingia siku yake ya pili hii leo nje ya hoteli alikohotubia kiongozi huyo.