Mfalme Mswati wa Swaziland abadilisha jina la taifa hilo
20 Aprili 2018Mabadiliko haya yanatangazwa katika wakati taifa hilo la kusini mwa Afrika likiadhimisha miaka 50 tangu lijinyakulie uhuru kutoka kwa Muingereza.
Mfalme huyo ameuita "Ufalme wa eSwatini" mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni- akihutubu kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2017 na pia katika Umoja wa Afrika na makongamano mengine ya kimataifa.
Akihutubia umati mkubwa katika uwanja, kwenye mji mkubwa wa pili wa Manzini, kilomita 40 mashariki ya mji mkuu wa Mbambane, mfalme alisema Swaziland ilikuwa inarudisha jina lake la asili ambalo lilikuwa linatumika kabla ya kutawaliwa na Uingereza.
Taifa hilo maskini Kusini mwa Afrika- mwanachama wa Jumuiya ya Madola- lilipata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1968.
"Ningependa kutangaza kuwa, kuanzia leo, taifa hili Iitafahamika kuwa eSwatini," mfalme alisema.
Alisema jina Swaziland limesababisha suitafahamu. "Kila wakati tunapozuru nje ya nchi watu wanasema tunatokea Switzerland," mfalme aliongeza.
Mfalme, aliyekuwa kavalia mavazi ya kijeshi ya rangi nyekundu na nyeusi na kusafiri kwenye gari ambalo lililokuwa wazi, alisema, anataka taifa lake liwe na jina ambalo watu wake wanaweza kutambuliwa nalo.
Idadi kubwa ya watu ni maskini
Wengi wa watu wanaotawaliwa na mfalme huzumbua riziki kutokana na ukulima wa sukari. Kuna umaskini mkubwa kwenye taifa hilo lenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Ukimwi.
Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen alihudhuria hafla hiyo kwenye taifa hilo ambalo limedumisha mahusiano yake na Taiwana badala ya Uchina.
Ni mara ya kwanza kwa Tsai kuzuru Afrika tangu kuchukua usukani wa taifa hilo mwaka 2016.
Kama tu mataifa mengi Swaziland haikubadilisha jina lake baada ya kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza iliyoitawala kwa zaidi ya miaka 60.
Hatua ya kulibadilisha jina limekuwa likijadiliwa kwa miaka sasa, huku wabunge kadhaa wakijadili suala hilo mwaka 2015.
Idadi kubwa ya watu wana Ukimwi
Mfalme huyo aliyetawazwa mwaka 1986 akiwa na umri wa 18, anatawala kwa mkono wa chuma na mara nyingi amekosolewa kwa maisha yake ya anasa licha ya wananchi wake wengi kuishi katika umasikini.
Vyama vya kisiasa vimepigwa marufuku kushiriki kwenye uchaguzi, wagombeaji ambao wameidhinishwa na machifu pekee waliowatiifu kwa mfalme, ndio wanaoruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi.
Taifa hilo lenye idadi ya yumkini watu milioni 1.3 lina moja ya viwango vikubwa vya watu wanaosihi na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi huku asilimia 27 ya watu wazima wakiuguwa ugonjwa huo.
Kubadilishwa kwa jina hilo kunamaanisha kuwa katiba ya nchi hiyo itarekebishwa halikadhalika mabadiliko yafanyiwe idara yake ya jeshi la polisi, jeshi la ulinzi na Chuo Kikuu cha Swaziland.
Baada ya uhuru, Rhodesia ilibadilishwa kuwa Zimbabwe, Nyasaland ikawa Malawi, na Bechuanaland ikawa Botswana.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp, Reuters
Mhariri: Mohamed Khelef