Suva. Jeshi lachukua madaraka Fiji.
5 Desemba 2006Kamanda wa majeshi ya Fiji Frank Bainimarama amechukua udhibiti wa serikali ya nchi hiyo , ikiwa ni mapinduzi ya nne katika taifa hilo lililoko katika eneo la bahari ya Pacific katika muda wa chini ya miongo miwili.
Katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu Suva , Bainimarama amesema kuwa amechukua madaraka maalum chini ya katiba ya nchi hiyo ambayo inamruhusu kuchukua madaraka ya rais, na anayatumia madaraka hayo kumwachisha kazi waziri mkuu Laisenia Qarase na ameteua uongozi wa muda.
Amesema kuwa ataachia wadhifa huo wa urais wiki ijayo.
Uchaguzi ambao utarejesha demokrasia utafuatia baadaye baada ya kuundwa kwa serikali ya mpito.
Waziri mkuu wa zamani Qarase amesema kuwa amewekwa kizuizini nyumbani kwake , na kwamba alikuwa hana uwezo wa kulizuwia jeshi kuchukua madaraka.
Australia na New Zealand zimeshutumu mapinduzi hayo, na kusema kuwa hatua hizo zilizochukuliwa na jeshi ni kinyume na katiba.