Sura za Tete: Jimbo katika andasa za makaa
Tokea kugundulika kwa akiba kubwa ya makaa ya mawe, Tete, jimbo la kati la Msumbiji, limekuwa likivutia watu wengi kwa imani ya kutengeneza pesa kwa haraka. Lakini je, makaa hayo ya mawe yanaweza kutosheleza watu wote?.
Coque, mfanyakazi
Coque ana umri wa miaka 28 na tangu alipokuwa na miaka minne amekuwa akifanya kazi na kampuni ya migodi ya Uingreza na Australia ya "Beacon Hill" huko Tete, Msumbiji. Amekuwa akifanya kazi ya kuyapakia vizuri makaa ya mawe kwenye malori ambayo husafirishwa kwenda nchi jirani ya Malawi. Kwa gari moja analopakia hulipwa Meticais 800 (sarafu za Msumbiji) sawa na euro 20 ambazo hugawana na mwenzake.
Paulo, kiongozi wa kampuni ya Vale Msumbiji
Paulo Horta anasema "Miradi yetu inawasaidia wananchi". Kwa kupitia kampuni mpya, huduma na kodi za watu wengine pamoja na ajira. Vale yenyewe inafaidika kwa kupata msamaha wa kodi kwa vyoyote vile kodi ya kampuni hiyo iko ndogo kulinganishwa na fungu la kampuni nyengine zote zikichanganywa pamoja.
Gomes António, mhanga wa Ukatili
Gomes António Sopa hapo tarehe 10 mwezi wa Januari mwaka 2012 alikamatwa na kupigwa na polisi. Katika maandamano wakaazi walidai kuzingatiwa kwa ahadi walizopewa na Vale. Kampuni hiyo iligunduwa makaa ya mawe chini ya vijiji vyao na kuwahamisha kwa kuahidi nyumba mpya, ajira na huduma bora za afya. Hadi hii leo Antonio amekuwa akipata maumivu kwa kipigo hicho cha polisi.
Duzéria, mwanamatibabu
Mkaazi wa makaazi mapya waliohamishiwa hapo tarehe 25 Septemba analalamika kwamba kampuni hiyo kwa kuwahamisha wamevuruga mila zao za jadi. Mwanamke huyo anasema kwa mfano wamewatibuwa mizimu yao kwa kushindwa kuwatengea nyumba yao kwenye mipango ya ujenzi.
Lória, mkuu wa kijiji
Hivi karibuni Lória na jamii yake watahamishwa na kampuni ya migodi ya Uingereza na Australia ya Rio Tinto ambayo tayari inachimba mgodi mwengine sehemu hiyo ya chini ya ardhi ambayo Lória aliirithi kutoka kwa baba yake. Kampuni hiyo pia imegunduwa makaa ya mawe kwenye ardhi hiyo lakini Lória anagoma kuiacha nyumba yake.
Guta, mfanyabiashara
Guta anashughulikia wafanyakazi 130 katika kampuni yake ya useremala iliosajiliwa na kampuni ya migodi. Yeye hakuhisi sana neema hizo za kiuchumi zinazotokana na kampuni kubwa. Anasema miradi ya makaa ya mawe inahitaji kima kikubwa cha vitu ambavyo yeye hawezi kuvipata. Aliwahi kuagiziwa milango 5,000 katika kipindi cha siku 60. Ilibidi aisamehe kazi hiyo.
Olivia, msusi
Olivia (kushoto) mwenye umri wa miaka 29 amefika Tete hapo mwaka 2008 kutoka Zimbabwe alikokukimbia kutokana na kupanda kwa gharama za maisha na baada ya kusikia kwamba Tete kuna fursa kubwa. Hivi anafanya kazi kama msusi katika soko kuu pamoja na shoga yake Faith pia hujipatia fedha kwa shughuli za kutengeneza makucha. Kwa siku moja anapata Meticias 500 hadi 1,000 sawa na euro 15 hadi 25.
Canelo, muuza njugu
Canelo anasema yeye ana miaka 11 na yuko darasa la pili, kila mchana huuza njugu katika barabara za Tete kumsaidia mama yake ambaye hana kazi pamoja na baba yake ambaye pia hana kazi. Kifuko kidogo bei yake ni Meticias mbili kama centi tano za euro. Kwa mifuko mikubwa anataka Meticias tano sawa na centi 12 za euro.
Cataqueta, mwanaharakati
Manuel Cataqueta alihamia Tete hapo mwaka 2001. Mtetezi huyo wa haki za binaadamu anajuwa namna ya kuishi na gharama za maisha zinazopanda kila wakati. Kwa muda mrefu amekuwa hawezi kuishi kwa anasa kutokana na fedha anazopata. Anaishi katika chumba kimoja katika fleti yake ndogo lakini hataki kuhama. Leo nyumba nzuri huko Tete inakodishwa kwa euro 4,000 kwa mwezi.
Júlio, mtu mwenye matumaini
Mwnamuziki Júlio Calengo anasema nafasi za kufanya biashara ni nzuri hivi sasa kwa sababu kampuni nyingi mpya zinakuja Tete. Lengo lake ni kuwa na kampuni ya kusafisha. Kwa hivi sasa kuna ofisi za kutosha, maduka na nyumba za kukodisha ambazo zinahitaji kusafishwa na kwa ajili hiyo kunahitajika mtaji wa kuwekeza.