1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Super Cup: BVB yaiangusha Bayern

Sekione Kitojo
4 Agosti 2019

(Borussia Dortmund  almaarufu BVB wameanza  na  ushindi  katika msimu  huu  mpya  kwa  kuizaba  Bayern Munich  kwa  mabao 2-0 na kunyakua  kombe  la  Super Cup  la  Ujerumani siku ya Jumamosi(03.08.2019).

https://p.dw.com/p/3NJ4s
Deutscher Super Cup - Borussia Dortmund - Bayern München
Picha: picture-alliance/dpa/G. Kirchner

Dortmund hawajaweka  siri  ya  kutaka  kufikisha  mwisho miaka saba  ya  ushindi  wa  Bayern  katika  Bundesliga na  makamu bingwa  hao  wa  msimu  uliopita wametuma  ujumbe  wa  mapema kwa  mahasimu  wao.

Fußball DFL Supercup 2019 | Borussia Dortmund v Bayern München
Mlinzi wa Bayern Jerome Boateng akikokota mpira wakati akizongwa na wachezaji wa DortmundPicha: AFP/Getty Images

Mhispania  Paco Alcacer  alipachika  bao  muda  mfupi  tu  mara timu  hizo  ziliporejea  kutoka  mapumziko kwa  kiki  safi  kutoka  nje ya  sanduku  la  adhabu na  chipukizi kutoka  England Jadon Sancho alikamilisha  ushindi  wa  Borussia  Dortmund  katika  shambulizi  la kushitukiza katika  dakika  ya  69.

Mabingwa  wa  mataji  mawili  katika  msimu  mmoja  Bayern wangeweza kusawazisha  muda  mfupi baadaye  lakini Marwin Hitz mlinda  mlango  wa  BVB  alifanikiwa  kuzuwia  juhudi  za  Kingsley Coman na  Manuel Akanji  aliondoa  mpira  uliopigwa  na  Thomas Mueller kabla  mpira  haujavuka  mstari  wa  goli.

Kombe  la  shirikisho  la  Ujerumani  duru  ya  kwanza  ni  wiki inayokuja kabla  ya  Bayern  kufungua  msimu  mpya  wa  Bundesliga ikiwa  nyumbani  dhidi  ya  Hertha BSC Berlin  hapo  Agosti 16.

Sebastian Kehl , mkuu  wa  kitengo  cha  wachezaji  wa  Dortmund , alikiambia  kituo  cha  utangazaji  cha  ZDF kwamba  Super Cup  ni "taji  ambalo  linaweza  kuwapatia  Dortmund msukumo, lakini  timu zote  mbili kwa  kweli  haziko  katika  kiwango  chake  cha  asilimia 100. Tunafahamu  kwamba  bado  tuna  changamoto  kubwa  katika mashindano  mbele  yetu."

Deutscher Super Cup - Borussia Dortmund - Bayern München
Pambano la DFL Super Cup nchini Ujerumani, Dortmund iliikandika Bayern mabao 2-0Picha: picture-alliance/dpa/M. Becker

Dortmund  ilitumia  fedha  nyingi  hivi  karibuni  lakini  mlinzi Nico Shulz alikuwa  mchezaji  pekee  aliyejiunga  msimu  huu  na  makamu bingwa  hao  aliyeonekana  katika  kikosi  cha  kwanza.

Mlinzi Mats Hummels  alikosa  pambano  hilo  dhidi  ya  klabu  yake ya  zamani  baada  ya  kupata  maumivu  mapema  siku  ya Jumamosi  wakati Julian Brandt , Thorgan Hazard  na  Mateu Morey pia  walikuwa  nje.

Nyota wa zamani

Lakini  nyota  wa  zamani  waliokuwa mara  moja  walionesha  uhai wakati Marco Reus  alipiga  kiki safi  ambayo  mlinda  mlango Manuel Neuer  wa  Bayern  aliuokoa kabla  ya  kukamilika  dakika  moja  ya mchezo  huo.

Alcacer  alikuwa  mara  nyingi  akitumika  kama  mchezaji  wa  akiba msimu  uliopita  lakini  alitumia  nafasi  zake  alizopata  mara  kadhaa na ndie  alikuwa  wa  kwanza  kufunja  mlango  wa  Bayern.

Deutscher Super Cup - Borussia Dortmund - Bayern München
Paco Alcacer aliyefunga bao la kwanza la DortmundPicha: Reuters/L. Kuegeler

Pasi  mbovu  ya  Thiago iliruhusu Sancho  kukatambuga  upande wa wingi  ya  kulia  na  Alcacer  alikutana  na  pasi  yake  na  kupiga mkwaju  wa  chini chini  uliomshinda  mlinda  mlango Manuel Neuer.

bayern  hawakuwa  na  mchezaji  Lucas Hernandez  ambaye  ni majeruhi  na  aliyenunuliwa  kwa  kitita  kikubwa  katika  historia  ya Bayern , wakati  Benjamin  Pavard  na  Fiete Arp walikuwa  katika benchi. Serge Gnabry  na  Javi Martinez  pia  wamepata  maumivu wakati  wakiwa  na  kikosi  chote  cha  zamani kilicheza  msimu uliopita.

"tumeshindwa  na  tumesikitishwa na  hilo,"  amesema  kocha  wa Bayern Nico Kovac, ambae  aliongeza  kwamba "hajafurahi" na uchezaji wa  timu  yake. "Hatukutumia  nafasi  tulizopata."

Kosa la  Thiago halikuwa  kosa  pekee walilofanya  wachezaji wa Bayern  hata  hivyo, na  Dortmund walipata  nafasi  nzuri  zaidi  kabla ya  kupata  bao  la  kuongoza.

Deutscher Super Cup - Borussia Dortmund - Bayern München
Kingsley Koman akipambana na wachezaji wawili wa BVB Omar Toprak (kushoto na Axel Witzel ( kulia)Picha: Reuters/L. Kuegeler

Alcacer  alipiga  mpira  kando  ya  lango  wakati  Neuer  alipokimbia kutoka  golini kwake  na  mlinda  mlango  huyo  wa  Ujerumani  pia alizuwia  mpira  wa  Raphael  Guerreiro  kabla  ya  mapumziko.

Hitz, aliyekaa  langoni  badala  ya  Roman Burki  aliyeumia , aliondoa hatari  iliyoletwa  na  Coman  wakati  mchezo  huo  ukiwa  sare  ya bila  kufungana  na  pia  alizuwia  juhudi  za  winga  huyo  wa Ufaransa  wakati  Bayern  ikitafuta  kusawazisha.