Sudan yautaka ujumbe wa UNITAMS kuondoka nchini humo
17 Novemba 2023Kaimu waziri wa mambo ya nje wa Sudan Ali Sadeq ameliandikia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuutaka ujumbe huo wa UNITAMS kuondoka nchini humo mara moja.
Katika barua hiyo iliyotumwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kusambazwa kwa baraza hilo la usalama, Sadeq ameuhakikishia Umoja huo kwamba serikali ya Sudan imejitolea kushirikiana kikamilifu na baraza hilo pamoja na makao makuu ya Umoja huo wa Mataifa.
Utekelezaji malengo wa UNITAMS ni wa kukatisha tamaa.
Sadeq amesema kuwa madhumuni ya kuanzisha misheni hiyo ilikuwa kusaidia serikali ya mpito ya Sudan baada ya mapinduzi ya Desemba 2018 na kuongeza kuwa utendakazi wa ujumbe huo katika kutekeleza malengo yake ni wa kukatisha tamaa.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa Sudan, msemaji wa Guterres Stephane Dujarric, amesema barua hiyo imepokelewa na kuwasilishwa kwa baraza hilo la usalama.