Sudan yasaini makubaliano ya kisiasa
17 Julai 2019Kuundwa kwa utawala wa kiraia lilikuwa ni dai kuu la waandamanaji walioshinikiza kuondolewa kwa baraza la kijeshi lililoshika mamlaka baada ya kuondolewa rais Omar al-Bashir, hatua iliyozusha mkwamo wa kisiasa nchini Sudan.
Msuluhishi mkuu kutoka kwa Umoja wa Afrika Mohamed Hassan Ould Labat amewaambia waandishi wa habari kwamba baraza hilo la kijeshi, TMC na kundi kuu la upinzani la Forces for Freedom and Change, FFC yamekubaliana kupokezana madaraka kwa kipindi cha miaka mitatu.
Makubaliano hayo ya kisiasa yanafungua njia ya enzi mpya kwa watu wa Sudan na kulingana na Labat ni hatua muhimu katika mchakato wa amani nchini humo.
Makamu mwenyekiti wa TMC Mohamed Dagalo ameyaelezea makubaliano hayo kuwa ni matokeo ya majadiliano magumu na ya muda mrefu huku mwakilishi wa kundi la FCC akiwaambia waandishi wa habari kwamba wanadhani kusainiwa kwa makubaliano hayo ya leo kunaashiria hatua moja mbele ya kufikia malengo ya mapinduzi.
Dagalo alisema "Nina furaha kuwatakia kila lenye heri raia wa Sudan na kutangaza kusainiwa kwa makubalino kati ya baraza la kijeshi na kundi la FFC, hatua inayoonekana kuwa ya kihistoria kwa watu wa Sudan."
Makubaliano ya kusaini waraka wa kikatiba kufanyika Ijumaa.
Kulingana na pande hizo, makubaliano haya yanajumuisha masharti ya uundwaji wa serikali ya baadaye ya Sudan kipindi cha miaka mitatu ya mpito mipango ya mageuzi ya kiuchumi na misaada ya kiutu.
Hata hivyo pande hizo bado zina kibarua cha kusaini waraka wa kikatiba ambao utaainisha kwa uwazi jukumu na mamlaka ya serikali mpya ya mpito. Makubaliano ya kusainiwa kwa waraka huo huenda yakafanyika siku ya Ijumaa.
Kusainiwa kwa makubaliano haya kunakuja siku kadhaa baada ya TMC na FFC kusema wamefikia makubaliano mapana ya mchakato wa kuandaa uchaguzi mkuu, kugawana mamlaka na kuchunguza ghasia za hivi karibuni dhidi ya waandamanaji zilizosababisha vifo vya raia 128.
Kulingana na mwandishi wa habari wa AFP kumekuwa na mazungumzo ya kina usiku wa kuamkia leo kujadili vifungu vya makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika na wasuluhishi kutoka Ethiopia baada ya wiki moja ya kuanza upya mazungumzo yaliyositishwa kati ya makundi hayo.
Utawala huo wa kiraia utahusisha wawakilishi sita wa kiraia na watano kutoka baraza la kijeshi. Miongoni mwa wawakilishi wa kiraia, watano watatokea kwenye kundi hilo kuu la upinzani la FFC.
Jenerali wa kijeshi ataongoza serikali ya mpito kwa miezi 21 na baadaye kuchukuliwa na raia watakaoongoza kwa miezi 18, hii ikiwa ni kulingana na mfumo wa mkataba ulioafikiwa. Baada ya miaka mitatu, kutafanyika uchaguzi mkuu.