1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yanasa masanduku 72 ya silaha kutoka Ethiopia

6 Septemba 2021

Mamlaka nchini Sudan imenasa masanduku 72 ya silaha zilizowasili nchini humo kutoka Ethiopia kupitia usafiri wa ndege ambazo wanazishuku zilinuiwa kutumika katika uhalifu dhidi ya serikali ya nchi hiyo

https://p.dw.com/p/3zxxp
Schweiz Abstimmung EU-Waffengesetz
Picha: Reuters/D. Balibouse

Shehena hiyo inachunguzwa na kamati iliyopewa jukumu la kuivunja serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al- Bashir aliyeondolewa madarakani mnamo Aprili mwaka 2019 baada ya maandamano makubwa. Shirika hilo la SUNA lilinukuu ripoti ya kamati hiyo inayosema kuwa silaha hizo awali zilitumwa kutoka Urusi kuelekea nchini Ethiopia mnamo mwezi Mei mwaka 2019 na kuzuiwa na mamlaka kwa muda wa miaka miwili.

Shirika hilo limeendelea kunukuu ripoti hiyo iliyosema kuwa mamlaka nchini Ethiopia iliruhusu bila ya tahadhari ya mapema, usafirishaji wa shehena hiyo kuingia nchini Sudan. Shirika la SUNA pia limeripoti kuwa shehena hiyo ilikuwa imebeba silaha na miwani ya kusaidia kuona usiku, bila ya kutoa maelezo zaidi.

Mpokeaji wa silaha hizo hakubainishwa lakini kamati hiyo haikufutilia mbali uwezekano kwamba zilikusudiwa kupelekwa kwa wafuasi watiifu kwa iliyokuwa serikali ya Bashir ambao mamlaka nchini humo imewashtumu kwa kujaribu kuhujumu mabadiliko dhaifu ya taifa hilo kuelekea katika demokrasia. Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia Dina Mufti hakujibu kwa haraka ombi la tamko kutoka kwa ofisi hiyo.

Äthiopien Botschafter Dina Mufti
Dina Mufti - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya EthiopiaPicha: Press Office Ambassador Dina Mufti

Haya yanajiri wakati ambapo kuna mvutano kati ya mataifa hayo mawili ya Ethiopia na Sudan kuhusiana na hatua ya wakulima wa Ethiopia kutumia eneo la mpakani lenye rotuba ambalo Sudan inadai kumiliki.

Mataifa hayo mawili pia yamekuwa na msuguano kuhusu bwawa la Grand Ethiopian Renaissance katika mzozo wa kikanda unaoihusisha Misiri. Mwishoni mwa mwezi uliopita, maafisa wa Ethiopia walisema kuwa walitibua shambulio katika bwawa hilo kutoka kwa makundi yaliojihami ambayo yalipata mafunzo na kupewa silaha na Sudan. Sudan ilikanusha vikali madai hayo na kuyataja kutokuwa na msingi.

Ethiopia imekuwa ikikabiliwa na mzozo katika eneo lake la Kaskazini la Tigray tangu mwezi Novemba. Mapigano hayo yalisababisha malefu ya wakimbizi kukimbilia nchini Sudan. Sudan nayo imekuwa ikipitia kipindi dhaifu cha mpito tangu kuondolewa madarakani Rais Omar al-Bashir na kwa sasa, taifa hilo linaongozwa na baraza la pamoja la uongozi wa kijeshi na kiraia.