1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yamwondoa balozi wake Kenya baada ya ziara ya Dagalo

5 Januari 2024

Sudan imemrejesha nyumbani balozi wake nchini Kenya kufuatia ziara na kikao kati ya Rais William Ruto na kamanda wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo, kinachopingana na jeshi la Sudan chini ya Abdel Fattah al-Burhan.

https://p.dw.com/p/4atHM
Bendera ya Sudan juu ya mtutu wa bunduki
Sudan inaandamwa na mzozo tangu Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la taifa na kikosi cha wanamgambo wa RSFPicha: Umit Bektas/REUTERS

Kwenye taarifa iliyochapishwa na shirika rasmi la habari la SUNA, kaimu waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan Ali al-Sadiq, balozi huyo ameamriwa kurejea nyumbani ili kufanya majadiliano zaidi kufuatia mapokezi ya hasimu wao nchini Kenya.

Kwa mtazamo wake, matokeo ya majadiliano ndiyo yatakayoamua hatima ya uhusiano kati ya Sudan na Kenya.

Kamanda wa kikosi cha Rapid Support Forces, RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, alifanya kikao na Rais William Ruto siku ya Jumatano.

Hamdan ameyazuru kwa mara ya kwanza mataifa kadhaa ya Afrika tangu vita kuzuka Aprili mwaka uliopita. 

Ruto aliyasifu mazungumzo yake na Daglo mjini Nairobi

Kwa upande wake Rais William Ruto alichapisha picha za mkutano wao kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuelezea kuwa amepokea vizuri nia ya RSF na Dagalo ya kutaka kumaliza mapigano ya Sudan kupitia mazungumzo.

Kamanda wa kikosi cha RSF  Mohamed Hamdan Dagalo
Kamanda wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan DagaloPicha: AP/picture alliance

Kabla ya kuwasili Nairobi, Kamanda Hamdan Dagalo akiwa Sudan aliafiki kuwa wako tayari kwa mazungumzo ya amani walipotiliana saini makubaliano ya amani na muungano wa vyama vya kiraia.

"Tunaunyosha mkono wa amani. Kama wanataka amani, tunawakaraibisha. Hakuna kitakachotuondoa Khartoum isipokuwa amani," kamanda huyo alikaririwa akisema hivi karibuni.

Juhudi za kikanda za upatanishi na kusitisha mapigano bado hazijafua dafu. Ifahamike kuwa kamanda Hamdan Dagalo ameshayazuru mataifa ya Uganda, Ethiopia na Djibouti.

Duru zinaeleza kuwa kwa sasa amekutana na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mjini Pretoria.

Juhudi za kikanda na kimataifa bado hazijafanikiwa kumaliza mzozo

Sudan | Wad Madani | Mzozo kati ya RSF na jeshi la Sudan
Mgogoro wa Sudan umewalazimisha mamilioni ya watu kuikimbia nchi hiyo.Picha: AFP/Getty Images

Ziara hizo zinaripotiwa kuukirihi uongozi wa Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambao umeandamwa na uasi katika miezi ya hivi karibuni na kuuweka katika nafasi hatari kwenye jukwaa la kidiplomasia la kimataifa.

Itakumbukwa kuwa shirika la maendeleo ya kikanda kwenye eneo la pembe ya Afrika, IGAD, lililo na makao yake mjini Djibouti, linaongoza juhudi za upatanishi kati ya Kamanda Hamdan Dagalo na hasimu wake mkuu wa majeshi ya Sudan Abdel Fattah al Burhan.

Akiwa Nairobi, kikao kilichopangwa kufanyika na waandishi wa habari hakikufanyika.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa,vita hivyo vya nchini Sudan vimewaacha zaidi ya milioni 7 bila makaazi na wengine elfu 12,190 wameuawa.

Majenerali hao wawili hawajapata kukutana ana kwa ana tangu vita vilipozuka Sudan.