Sudan yamshikilia kiongozi wa zamani wa baraza la utawala
14 Februari 2022Kiongozi huyo anazuiliwa baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama hapo Jumapili.
Taarifa ya kukamatwa kwake imetolewa na chama chake cha Unionist Alliance katika tukio la hivi karibuni la kamatakamata tangu mapinduzi ya mwaka uliopita.
Chama hicho kimesema Al-Fekki alisimamishwa na maafisa wa usalama wakati alipokuwa akiendesha gari yake akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake katika mji mkuu, Khartoum.
Hii ni mara ya pili kwa Fekki kutiwa mbaroni tangu jeshi lilipotwaa madaraka Oktoba 25 mwaka uliopita likiongozwa na mkuu wa majeshi, Abdel Fattah al-Burhan, ambapo utawala wa kiraia uliondolewa na kuvuruga kipindi cha mpito kuelekea utawala kamili wa kiraia.
Wanachama wawili wa chama cha Unionist Alliance wameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwa masharti ya kutotajwa majina kwamba Fekki alipelekwa eneo lisilojulikana.
Fekki alikuwa mwanachama wa baraza lililoitawala Sudan ambalo liliiongoza nchi hiyo chini ya mkataba wa kugawana madaraka kati ya watawala wa kiraia na jeshi kufuatia kuondolewa kwa kiongozi wa muda mrefu, Omar al-Bashir.