1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la Zanzibar lafikishwa Umoja wa Mataifa

Mohammed Khelef20 Septemba 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amepokea tamko la maandishi kutoka Muungano wa Vyama vya Kiliberali Duniani kupitia Kikao cha 33 cha Baraza la Haki za Binaadamu juu ya mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar.

https://p.dw.com/p/1K5Yx
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.Picha: Getty Images/AFP/J. Samad

Tamko hilo lililopewa jina la "Wito kwa Ajili ya Demokrasia na Utawala wa Sheria Zanzibar" limekabidhiwa likiwa na vielelezo kadhaa vinavyoorodhesha matukio ya ukiukwaji wa haki za binaadamu na misingi ya utawala bora kwenye visiwa hivyo, vilivyo sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taifa kubwa kabisa kieneo katika eneo la Afrika Mashariki.

Akizungumza na Deustche Welle mchana wa leo (20 Septemba 2016) akiwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, kunakoendelea pia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja huo, Makamu wa Rais wa Muungano wa Vyama vya Kiliberali Duniani, Robert Woodthorpe, alisema umefika wakati sasa kwa taasisi hiyo kuu ya kilimwengu, kubeba jukumu la kuhakikisha Zanzibar na Tanzania zinaheshimu haki za binaadamu na misingi ya demokrasia.

"Tunautaka Umoja wa Mataifa kuchukuwa hatua kwa mambo yanayoendelea Tanzania kwa ujumla na makhsusi hasa kwa Zanzibar, kwa sababu tunaamini kuwa kuna uvunjaji wa wazi wa haki za binaadamu dhidi ya watu wa Zanzibar kwani uchaguzi halali ambao ulishuhudiwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika na waangalizi wengine ulifutwa kwa njia zisizo halali," alisema Woodthorpe.

Uvunjaji wa haki za binaadamu

Likitaja matukio kadhaa ya uvunjwaji wa haki za binaadamu kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa marudio wa Machi 20 mwaka huu visiwani Zanzibar, tamko hilo linasema kwamba Tanzania iliyosaini Mkataba wa Kilimwengu wa Haki za Binaadamu inapaswa kulinda haki za raia wake wote dhidi ya ubaguzi, vitisho, na kukamatwakamatwa ovyo kama vilivyo vifungu Namba 7 na 9 vya Mkataba huo.

Mgombea urais wa Zanzibar wa CUF mwaka 2015, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mgombea urais wa Zanzibar wa CUF mwaka 2015, Maalim Seif Sharif Hamad.Picha: DW/M. Khelef

Kwa mujibu wa tamko hilo, ambalo liliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia Ajenda Namba 3 ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja huo, inayohusu uimarishaji na ulinzi wa haki za binaadamu, kiraia, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, tangu kurejewa kwa uchaguzi wa Machi 20 mwaka huu, wananchi visiwani Zanzibar wanaishi kwa hofu, vitisho, mateso na ukiukwaji wa haki za binaadamu, hasa miongoni mwa wanachama wa vyama vya upinzani.

"Katika nchi kama Zanzibar, tunahofia kwamba uwezekano wa ghasia kuchochewa na serikali ni mkubwa, jambo ambalo linayaweka maisha ya watu hatarini. Sio ya wanasiasa pekee, bali watu wanaweza kupandwa na hasira na bila shaka kunaweza kuwako machafuko na watu wakapigwa risasi. Na tuna wasiwasi sana na maisha ya watu na haki yao ya kufaidi demokrasia," Woodthorpe aliiambia Deutsche Welle.

Wito wa majadiliano

Likizungumzia uchaguzi wenyewe wa marudio, tamko hilo linasema uchaguzi huo ambao uligomewa na chama kikuu cha upinzani visiwani humo, CUF, uliitishwa tu kwa lengo la makusudi la chama tawala, CCM, na aliyekuwa mgombea wake wa urais, Dk. Ali Mohamed Shein, "kung'ang'ania madaraka, kwa gharama za kuikanyaga misingi ya kidemokrasia na mchakato wa chaguzi huru na haki."

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.Picha: DW/M. Khelef

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 28 Oktoba 2015, siku tatu baada ya kumalizika kwa upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo, Jecha Salim Jecha, aliufuta uchaguzi huo, ambao chama cha CUF kilisema mgombea wake urais, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa ameshinda kwa asilimia 53, na kisha kuitisha mwengine Machi 20 mwaka huu.

Tangu wakati huo, mkwamo mwengine wa kisiasa umevikumba visiwa hivyo maarufu kwa utalii kwenye Bahari ya Hindi, na hadi sasa jitihada za kuukwamua hazijaonekana kupata mafanikio.

Hata hivyo, kupitia tamko lao hilo kwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Muungano huu wa vyama vya kiliberali duniani unasema wakati wa kuzungumza na kuyamaliza ni sasa, licha ya kuvunjwa moyo na upande wa serikali ambao umegomea majadiliano.

"Tunaamini, chini ya wajibu wa kulinda, ni lazima kuzungumza kabla ya kuchukuwa hatua yoyote. Tunahisi kunapaswa kuwako majadiliano ndani ya Tanzania na pia Zanzibar, lakini jambo la kushangaza ni kuwa Rais (John Magufuli wa Tanzania) ameamua kuwa hataki majadiliano yoyote yale na anafikiri kulichukulia suala hili kwa ukali. Hatari ni kuwa ameanza kuzungumzia kuwakamata watu, hali inayotaka kufanana na ya Burundi," alisema Woodthorpe.

Miongoni mwa vyama vinavyounda muungano huu wa kiliberali ni chama cha Democrat cha Rais Barack Obama wa Marekani, DA cha Afrika Kusini, chama tawala nchini Senegal na CUF.

Mwandishi: Mohammed Khelef/UN
Mhariri: Iddi Ssessanga