1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la wakimbizi lahanikiza magazetini

Oumilkheir Hamidou
21 Julai 2017

Suala la wakimbizi ndio mada kuu iliyogonga vichwa vya habari vya  magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii ingawa mradi wa pamoja kati ya wataalam wa Ujerumani na Afrika nao pia umezingatiwa.

https://p.dw.com/p/2gyIJ
Italien Flüchtlinge auf dem Mittelmeer
Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Tunaanza na mada iliyohanikiza wiki hii magazetini: Wakimbizi: Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika jinsi wataliana wanavyokabiliana na wimbi la wakimbizi wanaozidi kuongezeka kutoka Afrika. Gazeti linazungumzia nafasi ya kuchaguliwa upya Giovanni Corbo, meya wa  mji mdogo wenye wakaazi 5500-Besnate katika mkoa wa Lombardie, uchaguzi utakapoitishwa tena. Chanzo ni msimamo wake kuelekea wakimbizi. Msimamo huo umewafanya wengi kutikisa kichwa hata wale miongoni mwa wafuasi wa chama chake mwenyewe cha Social Democrat PD. Anatishia kugoma kula chakula. Sababu ni kwamba wizara ya mambo ya ndani mjini Roma imepanga wakimbizi 15 wapelekwe katika mji huo mdogo, lakini mwishoe anajikuta na wakimbizi 32 anaobidi kuwahudumia, amelalamika mwanasiasa huyo wa chama cha waziri mkuu wa zamani Matteo Renzi kupitia mtandao wa kijamii Facebook anaetaka maamuzi yaliyopitishwa yatekelezwe.

Hata hivyo lakini uamuzi wake wa kugoma kula chakula, umekosolewa na sehemu kubwa ya wataliana na hasa kutoka Sicilia na Apulia wanaosema hiyo si sababu ya kuyatia hatarini maisha yake. Katika majimbo hayo hasa kuna maeneo ambayo wakimbizi wanapokelewa mikono miwili kasababu wanasaidia kuchangamsha hali ya maisha na kuleta neema..

Frankfurter Allgemeine linanukuu ripoti ya umoja wa mataifa inayosema wakimbizi 171.000 wamengia Italia mwaka jana na kuashiria idadi yao huenda aikawa sawa na hioyo kwaamwaka huu wa 2017.

Wamoroko wanazidi kuihama nchi yao na kuingia Ulaya

Lilikuwa gazeti hilo hilo la Frankfurter Allgemeine lililozungumzia kuhusu  wimbi jengine la wakimbizi-kutoka Afrika. Safari hii wanayatia hatarini maisha yao ili wawasili Uhispania. Gazeti linazungumzia kisa cha wakimbizi 52 waliojazana ndani ya mashua za mpira mapema mwezi huu wakitokea Moroko . Watatu tu ndio walioweza kuokolewa na walinzi wa bahari ya Uhispania. 49 wamezama. Ni hasara kubwa kabisa ya maisha kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, linaandika Frankfurter Allgemeine lililonukuu halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayowahudumia wakimbizi ikisema. Idadi ya wahanga inazidi kuongezeka kwasababu watu wanaotokea Moroko na Algeria na ambo wanataka kuja Ulaya inazidi kuongezeka pia. Na sio tu kupitia baharini wengine wanayatia hatarini maisha yao kwa kuparamia  ukuta uliozungushwa senyenge  unaoigawa Maroko na maeneo ya Uhispania ya Ceuta na Melilla. Licha ya juhudi za vikosi vya usalama vya Moroko kuwazuwia wakimbizi hao, Frankfurter Allgemeine linasema mikururo ya wakimbizi na hasa kutoka Moroko wanazidi kuongezeka.

Changamoto isiyokuwa na mfano

Nalo gazeti la mjini Berlin, die tageszeitung limezungumzia mahojiano waliyokuwa nayo na mwana social Democrat Christian Ude aliyeandika kitabu kuhusu wakimbizi-kitabu alichokipa jina "Changamoto ya karne". Katika kitabu hicho Christian Ude anakosoa msimamo  anaoutaja kuwa wa hadaa wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke kuelekea wakimbizi na kuunga mkono fikra ya kuanzishwa mpango wa waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller wa kuhimiza maendeleo Marshallplan barani Afrika.

Raslimali mbadala na endelevu kwa Afrika

Mada yetu ya pili na ya mwisho magazetini inahusiana na mradi wa pamoja  ulioanzishwa na mtandao wa wataalam wa Ujerumani na Afrika kuhusu matumizi endelevu ya mabaki ya mimea na wanyama."Rasli mali ambayo haikuguswa" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Bonn, General Anzeiger linalozungumzia kuhusu mradi huo. Gazeti linataja ripoti ya Umoja wa mataifa inayokadiria idadi ya wakaazi wa eneo la Afrika kusini mwa jangwa la sahara itaongezeka takriban mada dufu hadi ifikapo mwaka 2050. Na ili chakula cha kutosha kiweze kulimwa, maeneo ya kilimo yatabidi yapanuliwe na mazao yazidishwe. Katika maeneo wanakoishi watu kwa wingi Afrika Magharibi na mashariki mwa Afrika, mfano nchini Ghana, Nigeria au Ethiopia azma hiyo haitekelezeki.

Ndio maana kuna umuhimu wa kutengeneza Biomasse, yaani rasli mai inayotokana na mimea, wanyama na mabaki yao ambayo ni endelevu na ambayo hadi wakati huu hayajatumika vya kutosha. Wataalam wa kituo cha utafiti wa maendeleo katika chuo kikuu cha Bonn ZEF wanashirikiana na wenzao wa shirika la utafiti wa shughuli za kilimo barani Afrika-Fara  na kuanzisha mtandao wa kwanza wa aina yake kuhusu matumitzi endeleu ya raslimali hiyo. Wataalam mia 100 kutoka Ujerumani na Afrika wanakutana mjini Bonn kuanzisha mtandao huo utakaojishughulisha na fani tofauti. General Anzeiger linakumbusha kwa miaka sasa wataalam wa kituo cha ZEF wamekuwa wakijishughulisha na namna ya kudhamini usalama wa chakula barani Afrika.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri. Mohammed Khelef