1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la uhamiaji laugawa muungano wa Kihafidhina wa Merkel

6 Septemba 2015

Uamuzi wa Kansela Angela Merkel kuruhusu maelfu ya wahamiaji waliokwama Hungary kuingia Ujerumani umesababisha mpasuko katika muungano wake wa kihafidhina akituhumiwa na chama cha CSU kwa kutuma ishara ya makosa Ulaya

https://p.dw.com/p/1GRuT
Wahamiaji nchini Hungary wakiwa na picha za Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Wahamiaji nchini Hungary wakiwa na picha za Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters/B. Szabo

Mzozo huo umeibuka baada ya Ujerumani na Austria kufunguwa mipaka yao kwa maelfu ya wahamiaji waliokumbwa na uchovu waliopelekwa mpakani mwa Hungary kwa safari hizo na serikali ya mrengo wa kulia ya nchi hiyo iliogoma kuwapokea.

Ujerumani inatarajia kupokea wahamiaji 800,000 mwaka huu ambayo ni idadi kubwa kabisa kuwahi kupokelewa na nchi za Umoja wa Ulaya.Hapo mwezi wa Augusti pekee zaidi ya watafuta hifadhi 100,000 wamesajiliwa nchini humo.

Taifa hilo kubwa lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya linawavutia wahamiaji wengi ambao mara nyingi tayari wanakuwa na ndugu zao wanaoshi hapo.Merkel na Rais Viktor Orban wa Hungary walikubaliana katika mazungumzo yao ya simu kwamba uamuzi huo wa kuwapokea wakimbizi hao wengi kutokana na vita nchini Syria ni wa muda uliochukuliwa kutokana na sababu za kibinaadamu.

Tuhuma dhidi ya Merkel

Lakini waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann ambaye chama chake cha Christian Social Union (CSU) ni chama ndugu kwa chama cha Christian Demokratik CDU cha Kansela Angela Merkel katika chama tawala katika serikali ya mseto nchini Ujerumani kimemshutumu kwa kushinikiza kupokelewa kwa wahamiaji hao bila ya kuzishauri serikali za majimbo ambazo inabidi zikabiliane na wimbi hilo la wakimbizi.

Horst Seehofer Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria.
Horst Seehofer Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer na viongozi wengine wa chama CSU wamekubaliana katika mazungumzo ya simu kwamba uamuzi wa Merkel wa kuwaruhusu wahamiaji waliokwama Hungary kuingia nchini ni "uamuzi wa makosa uliotolewa na serikali kuu ya shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani."

Taarifa hizo zilizoripotiwa na gazeti mashuhuri la Bild am Sonntag zimethibitishwa na msemaji wa chama cha CSU Simon Rehak ambaye amesema chama chake hicho cha kihafidhina kitaliweka suala hilo kwenye agenda katika mkutano wa ngazi ya juu wa serikali ya mseto ya Ujerumani Jumapili jioni.

Wanaotetea uamuzi wa Merkel

Lakini chama cha sera za mrengo wa wastani kushoto cha Social Demokratik SPD ambacho ni mshirika mdogo katika serikali ya muungano mkuu ya Merkel kinamtetea kiongozi huyo ambapo katibu Mkuu wa chama hicho Yasmin Fahimi ameuita uamuzi huo wa Merkel kuwa ni hatua pekee sahihi kuchukuliwa.

Katibu Mkuu wa chama cha SPD Yasmin Fahimi.
Katibu Mkuu wa chama cha SPD Yasmin Fahimi.Picha: picture-alliance/dpa

Amesema inabidi watowe ishara nzito ya ubinaadamu kuonyesha kwamba maadili ya Ulaya pia yana thamani wakati wa shida kwamba jinsi Hungary ilivyoshughulikia mzozo huo ni jambo lisilovumilika.Fahimi alikuwa akikusudia hatua ya Hungary ya kujaribu kuwazuwiya wahamiaji kwenye makambi na malumbano kati ya wahamiaji na polisi wa nchi hiyo.

Gazeti la Bild am Sonntag limeonekana kuiunga mkono hoja hiyo kwa kichwa cha habari " Merkel akomesha aibu ya Budapest."

Uchunguzi wa maoni ya wananchi wiki iliopita umeonyesha umashuhuri wa Merkel umeshuka kutokana na jinsi alivyoushughulikia mzozo huo wa wakimbizi lakini Wajerumani wengi hawana wasi wasi wa kumiminika kwa wakimbizi nchini mwao.

Agenda za mjadala

Serikali ya mseto ya Merkel inatarajiwa kukubaliana juu ya hatua kadhaa baadae Jumapili ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu kurahisisha ujenzi wa vituo vya watafuta hifadhi, kuongeza michango ya fedha kwa serikali za majimbo na miji pamoja na kuharakisha mchakato wa kuomba hifadhi.

Wahamiaji wakiwasili Munich,Ujerumani na kukaribishwa kwa mapokezi mazuri . (05.09.2015)
Wahamiaji wakiwasili Munich,Ujerumani na kukaribishwa kwa mapokezi mazuri . (05.09.2015)Picha: Getty Images/A. Beier

Agenda itajumuisha kutanuwa orodha ya nchi ambazo zinahesabiwa kuwa salama ikiimanisha kwamba raia wake hawana haki ya kuomba hifadhi yumkini nchi kama vile Kosovo, Albania na Montenegro. Miongoni mwa nchi ambazo tayari zinahesabiwa kuwa ni salama ni Serbia,Macedonia na Bosnia.

Serikali ya Ujerumani inataka kuharakishwa kwa mchakato wa kuomba hifadhi na kurudishwa makwao kwa wahamiaji wasiostahiki hususan wanaotokea kusini mashariki mwa Ulaya ili kuweka zingatio kwa wakimbizi wa vita kutoka nchi kama vile Syria,Iraq na Afghanistan.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/dpa

Mhariri : Yusra Buwayhid