1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stoltenberg ataka NATO ijiimarishe dhidi ya COVID-19

1 Aprili 2020

Katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg amesema ushirika huo unapaswa kuzuia janga la virusi vya corona kugeuka kuwa tishio la usalama na kuonya Urusi au makundi ya kigaidi huenda yakatumia vibaya janga hilo. 

https://p.dw.com/p/3aJg4
Belgien Brüssel NATO Generalsekretär Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Jens Stoltenberg ameongeza kuwa ni muhimu kwamba jumuiya hiyo inaposhughulikia janga la virusi vya corona, iendelee kutekeleza shughuli zake kwasababu vitisho na changamoto zilizopo hazipotei kwasababu ya virusi hivyo.

Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka jumuiya hiyo yenye mataifa wanachama 30, watafanya mazungumzo yao kesho Alhamisi kwa njia ya vidio, kujadili mwitikio wao kwa janga la ugonjwa wa COVID-19 ambao umesababisha vifo vya takriban watu elfu 30 barani Ulaya pekee.

Mawaziri hao wanatarajiwa kutoa taarifa ya pamoja kama njia ya kuonyesha umoja na kutuma onyo kwa wanaoonekana kuwa mahasimu kama vile Urusi kwamba jamii hiyo bado ina uwezo na iko tayari kujibu vitisho vyovyote.

Idadi ya vifo yaongezeka Uhispania

Spanien Corona-Pandemie
Picha: picture-alliance/dpa/E. Sanz

Wakati huo huo wizara ya afya nchini Uhispania imesema leo kuwa nchi hiyo imerekodi vifo 864 kutokana na maambukizi ya virusi vya corona katika muda wa masaa 24, hii ikiwa idadi ya juu zaidi ya vifo vilivyorekodiwa katika muda huo.

Hii ni siku ya tano mfululizo ambapo zaidi ya vifo 800 vimerekodiwa katika nchi hiyo ambayo imeathirika pakubwa kufuatia janga la virusi hivyo na kuongeza idadi ya vifo nchini humo kufikia 9,053.

Wakati huo huo, visa vipya vya maambukizi viliongezeka kwa 8000 na kuongeza idadi jumla ya maambukizi iliyorekodiwa kufika 102, 000. Pia wagonjwa 3500 waliokuwa wamedhibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi hivyo, wameruhusiwa kutoka hospitalini.

Zaidi ya watu elfu 22 kati ya watu elfu 51 waliotibiwa katika hospitali nchini Uhispania kutokana na ugonjwa wa COVID-19 wamepona.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaonya kuhusu kitisho cha upungufu wa chakula

FAO-Bericht | Frauen sind der Schlüssel zur Umkehrung des Verlusts an biologischer Vielfalt
Picha: FAO/Giuseppe Bizzarri

Katika hatua nyingine mkuu wa shirika la kilimo na chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Qu Dongyu, mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus na mkurugenzi mkuu wa shirika la biashara duniani (WTO)  Roberto Azevedo wameonya leo juu ya uhaba mkubwa wa chakula unaoelekea kuikumba dunia, iwapo serikali zitashindwa kusimamia vizuri mzozo unaoendelea wa virusi vya corona.

Serikali nyingi kote duniani zimetoa amri ya raia wake kubaki majumbani na kusababisha kupungua kwa kasi ya biashara ya kimataifa na usambazaji chakula.

Watu wananunua bidhaa kwa wingi kutokana na hofu na kuonyesha tayari kulemewa kwa hatua za usambazaji chakula huku maduka ya kujihudumia yakisalia na rafu tupu katika mataifa mengi.

Taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na viongozi hao, imesema kuwa kutokuwa na uhakika wa kupatikana kwa chakula huenda kukachochea wimbi la vikwazo vya kuuza chakula nje na kusababisha nakisi kwenye soko la kimataifa.