1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

urusi

Abdu Said Mtullya15 Februari 2014

Waziri Steinmeier amesema ni watu wa Ukraine tu wanaopaswa kuutatua mgogoro wao Waziri Steinmeier ameyasema hayo mjini Moscow katika ziara yake ya nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/1B90g
Frank-Walter Steinmeier bei Sergej Lawrow in Moskau
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kushoto)na mwenzake wa Urusi Sergei LawrovPicha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani aliwaambia waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov mjini Moscow kwamba hakuna atakaenufaika na kuwaka moto kwa Ukraine. Steinemeier amesema Ukraine asilani isigeuzwe kuwa kete katika mchezo wa sataranji. Waziri huyo wa Ujerumani ametamka kwamba ni juu ya pande zinazopingana nchini humo kutafuta suluhisho.

Akizungumza kwenye mkutano huo huo na waandishi wa habari, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aliulaumu Umoja wa Ulaya kwa kujaribu kujitanua karibu na mipaka ya Urusi kwa kuishinikiza Ukraine ichague kuwa na uhusiano na Umoja huo kwa kuuathiri uhusiano wa nchi hiyo na Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Lavrov aliyasisitiza madai ya nchi yake juu ya ujiingizaji wa nchi za magharibi katika mambo ya ndani ya Ukraine ambayo sasa inakabiliwa na mgogoro mkubwa.

Urusi na Umoja wa Ulaya zavutana

Urusi na Umoja wa Umoja wa Ulaya zimekuwa zinatupiana lawama tokea Ukraine, mnamo mwezi wa Novemba iamue kuiahirisha hatua ya kuutia saini mkataba wa biashara na Umoja wa Ulaya na badala yake kuamua kuuimarisha uhusiano wake na Urusi.Umamuzi huo ulichochea maandamano makubwa ya wananchi nchini Ukraine.Maandamano hayo yameshasababisha vifo vya watu sita na kuondolewa kwa Waziri mkuu.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Lavrov amezionya nchi za magharibi dhidi ya kujifanya waamuzi wa mgogoro wa Ukraine na amesema kuwa inapasa kuwaachia watu wa Ukraine wenyewe wautatue mgogoro wao. Lavrov amesema anakubaliana na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Steinmeier aliesema kwamba Ukraine isigeuzwe uwanja wa kupigania himaya za ushawishi.

Putin akutana na Steinmeier

Wakati huo huo, kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari cha Ujerumani, Rais Wladimir Putin amemwambia waziri wa Ujerumani Steinmeier kwamba Urusi inaunga mkono sera ya kuleta uhusiano wa karibu wa kiuchumi baina ya Ukraine na Umoja wa Ulaya. Putin amesema anaziunga mkono hatua za kuleta uhusiano huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anaefanya ziara ya siku mbili nchini Urusi amesema kuwa mazungumzo yake na Rais Putin yalikuwa na manufaa .Licha ya mgogoro wa Ukraine Steinmeier na Rais Putin walizungumzia juu ya uhusiano baina ya nchi zao.

Mwandishi:Mtullya Abdu rtre,afp,dpa,

Mhariri:Yusuf Saumu