Steinmeier ataka mtazamo mpya kuhusu Afrika
23 Februari 2015Waziri Frank-Walter Steinmeier amesema mtazamo kwamba Afrika ni bara la vita na migogoro unapaswa kubadilika, akiongeza kuwa ingawa bado mizozo ipo barani humo, lakini pia pia yapo maendeleo ambayo yanafaa kuwakilisha sura ya bara hilo. Hayo Steinmeier aliyasema mjini Nairobi, alikohitimisha ziara yake ambayo pia ilimfikisha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.
Kenya kwa upande wake imeitolea mwito Ujerumani kujenga viwanda zaidi kama hatua mojawapo ya kupanua uchumi wa nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika. Wito huo umetolewa na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni na biashara ya kimataifa nchini Kenya Bi Amina Mohammed alipokutana na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier mjini Nairobi.
Wito wa uwekezaji zaidi
Kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya kufanya mashauri ya kina na waziri mwenzake wa Ujerumani Walter Steinmeire, Waziri Amina Mohammed alisema huu ni wakati mzuri kwa Ujerumani kuwekeza nchini Kenya.
''Kuna zaidi ya viwanda mia moja tayari vya ujerumani hapa nchini Kenya na tunawaambia wengine pia waje. Tunahitaji viwanda vingi zaidi kutoka ujerumani kwani idadi ya ya wutu hapa sio tu milioni 44 bali kutokana na mikataba tuliyotia saini katika bala la Afrika tutakuwa na soko la kubwa zaidi ya watu milioni 600 kwa ujerumani katika eneo la Kusini, Mashariki na Afrika ya kati kushinda soko lake la Ulaya” Alisema Bi Amina Mohammed.
Miongoni mwa maswala yaliyojadiliwa ni usalama na amani katika eneo la Mashariki mwa afrika. Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier kwa upande wake allipongeza Kenya kwa juhudi zake za kuleta amani katika eneo la Mashariki mwa Afrika
Steinmeier alisema, “Niko hapa na mwakilishi wa sera za kigeni nchini Kenya. Tumekuwa na mazungumzo ya kina kuhusu ushirikiano wa kuleta uthabiti wa kimataifa. Nina furaha kuona jinsi Kenya imejitolea kusaidia mataifa jirani kusuluhisha mizozo kivita”
Mchango wa Kenya kwa amani wasifiwa
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani alisema nchi yake imejiloea kusaidia bara la Afrika kukua kiuchumi na kuipongeza Kenya kwa juhudi zake za kuleta amani katika eneo la mashariki mwa Afrika
“Tumekuwa tukijaribu kusaidia kwa kila njia kuleta uthabiti nchini Somalia kwanza kwa kuisadia Somalia kuwapa mafunzo maafisa wake usalama”. Alisema Steinmeier.
Kenya imekuwa ikisaidia nchi jirani kuleta uthabiti hasa nchini Somalia na Sudan Kusini.
“Nchini Somalia kunao wanajeshi wetu na tuaendelea kuisaidia Somali kama tulivyofanya mbeleni. Kuhusu Sudan Kusini tumefikia wakati ambapo harakati za kuleta amani nchini zinaendelea kwa kasi”. Aliongeza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya.
Waziri Steinmeier aliwasili mjini Nairobi jumamosi jioni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alikopitia kwenye ziara yake iliyomalizika nchini Kenya .
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani alifanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta na kisha kukutana na viongozi wa upinzani kabla kufanya mashauriano na Jaji Mkuu Dr. Willy Mutunga. Steinmeire alikuwa ameandamana na wakurugenzi 20 wa kampuni mbalimbali nchini Ujerumani.
Mwandishi: Alfred Kiti DW- Nairobi
Mhariri: Iddi Ssessanga