1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier aanza ziara nchini Ghana

11 Desemba 2017

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aanza ziara ya siku nne, anaanzia nchini Ghana halafu atakwenda Gambia. Hii ni ziara yake ya kwanza barani Afrika tangu ashike wadhifa wa urais kuanzia mwezi Machi.

https://p.dw.com/p/2p7pp
Rais wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier
Rais wa Ujerumani Frank Walter-SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Katika ziara hiyo rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameongozana na ujumbe wa watu 18 akiwemo waziri wa Uchumi Brigitte Zypries na wajasiriamali kadhaa. Masuala yatakayozingatiwa katika ziara hiyo ya rais wa Ujerumani na ujumbe wake ni uhusiano wa kiuchumi, kutafuta njia za kukabiliana na mambo yanayosabisha watu kuzikimbia nchi zao sambamba na kuwarudisha wakimbizi makwao.

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo
Rais wa Ghana Nana Akufo-AddoPicha: picture alliance/dpa/AP Photo/G. V. Wijngaert

Akizungumzia juu ya ziara hiyo ya rais wa Ujerumani kiongozi wa Ghana Nana Akufo-Addo amefafanua malengo ya nchi yake, amesema anataka kuiona Ghana ikijengwa bila kutegemea misaada, anapendelea pia Ghana iliyo huru na inayojisimamia yenyewe. Rais Akufo-Addo amesema yote hayo yanaweza kutimizwa endapo Waghana watakuwa na mtazamo sahihi. Rais huyo wa Ghana amesema nchi yake pamoja na bara la Afrika hazipaswi kuendelea na sera  ya kutegemea hisani ya nchi za nje na amesisitiza umuhimu wa kujitegemea. Kiongozi huyo wa Ghana amesema mfumo wa ushirikiano wa maendeleo hadi sasa haujaleta mafanikio makubwa.

Hata hivyo Ghana itaendelea kushirikiana na nchi za Ulaya ili kusonga mbele. Swala hilo litatiliwa maanani katika ziara ya rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Katika kuunga mkono mageuzi ya Ghana, Ujerumani itatenga Euro milioni 100 kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo katika kuyaboresha mazingira ili kuwavutia wawekezaji vitega uchumi kutoka nje na ndani ya nchi hiyo.

Rais wa tume ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker
Rais wa tume ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Reuters/D. Pignatelli

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya utaipa Ghana msaada wa Euro milioni 323 hadi kufikia mwaka wa 2020. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuendeleza utawala bora, elimu, maendeleo ya kijamii na katika sekta ya kilimo. Ghana nchi yenye watu milioni 29 kwa miaka kadhaa imekuwa inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa ajira na matatizo ya nishati.Tangu aingie madarakani mnamo mwezi Januari rais Nana Akufo Addo ametekeleza sera za mageuzi.

Mwandishi: Zainab Aziz/Borchers, Jens / Rabat (HR)

Mhariri: Grace Patricia Kabogo