1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouawa Sri Lanka wafika 290, hali ya dharura yatangazwa

Daniel Gakuba
22 Aprili 2019

Rais wa Sri Lanka Maithripala Sirisena ametangaza hali ya dharura kuanzia saa sita usiku Jumatatu kufuatia shambulizi la kigaidi kwenye makanisha na hoteli za kifahari siku ya Pasaka. Idadi ya waliouawa yafika 290.

https://p.dw.com/p/3HDZS
Friends and relatives mourn for Mary Noman Shanthi, 58, and Rohan Marselas Wimanna, 59, who died as bomb blasts ripped through churches and luxury hotels on Easter, in Negombo
Picha: Reuters/A. Perawongmetha

 

Taarifa ya Kitengo cha habari cha serikali ya Sri Lanka imesema, ''Serikali imeamua kutangaza sheria inayolenga kuzuia ugaidi ambayo itaanza kuheshimiwa saa sita usiku leo.'' Taarifa hiyo imefafanua kuwa hatua hiyo itahusiana tu na shughuli za kuzuia ugaidi, na haitaingilia uhuru wa watu wa kutoa mawazo yao.

Msemaji wa serikali mjini Colombo Rajitha Senaratne amesema kuwa serikali ya Sri Lanka inaamini kuwa kundi lenye itikadi kali la nchini humo lijulikanalo kama NTJ (Nationa Thowheeth Jama'ath) ndilo limefanya shambulizi hilo, na ameongeza kuwa uchunguzi ulikuwa ukifanyika kuangalia iwapo kundi hilo lilipata usaidizi kutoka nje ya nchi.

Polisi ilitoa onyo la mapema

Sri Lanka Anschlag Terror Ostern
Majonzi ni makubwa kwa waliopoteza wapendwa waoPicha: Reuters/A. Perawongmetha

Nyaraka zilizoonwa na shirika la habari la AFP zinaonyesha kuwa polisi ya Sri Lanka ilitoa onyo mnamo Aprili 11. kwamba shirika la kijasusi la nchi ya kigeni lilikuwa limeripoti kwamba NTJ ilikuwa ikiandaa njama ya kushambulia makanisha na ubalozi wa India.

Hakuna mengi yanayojulikana kuhusu kundi la NTJ, mbalo siku za nyuma lilihusishwa na kufanya uharibifu kwenye sanamu za madhehebu ya Buddha. Chanzo cha habari kutoka jeshi la polisi kimeeleza kuwa watu 24 waliokwishakamatwa wakishukiwa kuhusika na mashambulizi ya siku ya Pasaka wanayo mafungamano na kundi hilo lakini hakufafanua zaidi.

Kufuatia shambulizi hilo la umwagaji mkubwa wa damu, Sri Lanka iliifunga mitandao mingi ya kijamii, ikiwemo Whatsapp na Facebook, hatua inayodhihirisha kupungua kwa imani katika makampuni hayo mawili makubwa ya kimarekani, kuweza kuchuja taarifa za uchochezi. Mitandao hiyo miwili pamoja na Instagram imeshutumiwa kusambaza habari za uongo. Mtandao wa twitter haukuathiriwa na hatua hiyo.

Ghasia za kidini

Serikali ilihofu kuwa kuenea kwa ujumbe wenye hasira kungechochea ghasia zaidi nchini Sri Lanka, kisiwa ambacho wakazi wengi wa Wabuddha, lakini pia yakiwepo makundi ya makubwa ya Waislamu, Wakristo na Wahindu. Historia ya kisiwa hicho imejaa makovu yaliyoachwa na vurugu za kidini.

Hii si mara ya kwanza kwa Sri Lanka kuifunga mitandao ya kijamii. Machi 2018 serikali ya nchi hiyo iliizuia kwa wiki nzima mitandao ya Whatsapp, Facebook na mitandao mingine, kwa hofu kwamba ilikuwa ikiendeleza kampeni ya chuki dhidi ya Waislamu katika jimbo la katikati mwa nchi hiyo.

afpe, ape, rtre