1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi, aendelea na ziara yake Mashariki ya Kati.

Omar Babu5 Aprili 2007

Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi, ameendelea na ziara yake ya Mashariki ya Kati ambapo amekutana na Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia. Bi Nancy Pelosi aliwasili mjini Riyadh jana akitokea Syria alikoshauriana na Rais Bashar Al- Assad.

https://p.dw.com/p/CHGs
Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi akutana na wajumbe wa Baraza la Shura nchini Saudia Arabia.
Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi akutana na wajumbe wa Baraza la Shura nchini Saudia Arabia.Picha: AP

Bi Nancy Pelosi alikutana na mfalme Abdullah katika mji wa Janadriyah kiasi kilomita arobaini kaskazini Mashariki mwa mji mkuu Riyadh.

Ziara hiyo ya Bi Nancy Pelosi katika eneo la Mashariki ya Kati imepingwa vikali na serikali ya Rais George W Bush hususan hatua yake ya kushauriana ana kwa ana na Rais Bashar al-Assad wa Syria, ambaye kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikimchukulia kuwa mzizi wa fitina katika eneo hilo.

Bi Pelosi amekaidi shutuma zote zilizolimbikiziwa ziara hiyo na akajasiri kushauriana na kiongozi huyo wa Syria.

Ama Spika huyo alionekana mwingi wa matumaini baada ya mashauriano yake na wakuu wa Syria. Bi Pelosi alisema:

"Ninaamini mkutano wetu umefana. Tumeshauriana na wakuu wa Syria kwa njia ya kirafiki.

Tuliwasili hapa kwa njia ya urafiki na pia wingi wa matumaini.Tuna imani kwamba Syria itakuwa kichocheo cha kupatikana amani"

Spika huyo wa bunge la Marekani amepangiwa kukutana na wanachama wa baraza la Shura la Saudi Arabia ambalo lina wanachama mia moja na hamsini, wote wanaume.

Hata hivyo Bi Pelosi hatarajiwi kulihutubia baraza hilo kama walivyowahi kufanya baadhi ya viongozi wa kigeni, lakini atajumuika na baadhi ya wanachama hao kwa dhifa ya chakula cha mchana.

Wakati Bi Pelosi anapoendelea na ziara yake katika Mashariki ya Kati, nyumbani ameshutumiwa vikali na serikali yake ambayo inasema Syria imesababisha maafa chungu nzima kwa kuwafadhili wanamgambo wenye misimamo mikali.

Makamu wa Rais wa Marekani, Dick Cheney amekiambia kituo kimoja cha Redio kwamba ziara hiyo inatatiza juhudi za Marekani za kumtenga Rais Bashar al-Assad.

Vinginevyo, kwa mujibu wa Dick Cheney, ziara ya Bi Pelosi ni sawa na kumpongeza Bashar al-Assad kwa kujihusisha na mambo ya ndani ya Lubnaan, Iraq na kwengineko.

Spika huyo wa Bunge la Marekani, ambaye ndiye afisa mkuu wa kwanza wa Marekani kuitemebelea Syria miaka ya karibuni hajazingatia shutuma dhidi yake.

Badala yake amehoji sababu ya ziara yake kuzua tumbo joto kiasi hicho ilhali hivi karibuni baadhi ya washirika wa Rais George W Bush kutoka chama cha Republican waliitembelea Syria wala hapakuwa na shutuma zozote dhidi yao.

Bi Pelosi alisema ziara yake ilipangwa kutokana na mapendekezo ya tume ya Rais Bush kuhusu Iraq kwamba Syria na Iran zijumuishwe katika harakati za kumaliza ghasia zinazoendelea nchini Iraq.