Spika wa baraza la seneti DRC ajiuzulu
5 Februari 2021Hatua hiyo ndiyo ya hivi karibuni inayochukuliwa na kambi ya rais Felix Tshisekedi kuwaengua washirika wa mtangulizi wake, Joseph Kabila
Spika wa baraza la seneti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Alexis Thambwe Mwamba amewasilisha barua yake ya kujiuzulu leo, katika hatua ya hivi karibuni inayochukuliwa na kambi ya rais Felix Tshisekedi kuwaengua washirika wa mtangulizi wake, Joseph Kabila.
Katika barua hiyo kwa ofisi ya ukaguzi wa seneti, ambayo nakala yake imeonekana na shirika la habari la AFP, Thambwe Mwamba amesema ''hakuna tena hali ya kuaminiana baina yake na kundi la maseneta''.
Kwa maneno hayo alikuwa akimaanisha kundi la wajumbe wengi wa baraza la seneti ambao waliweka shauri la kutokuwa na imani naye na kumtaka aondoke katika wadhifa wake.
Vigogo wengi washirika wa rais wa zamani wamekuwa wakipoteza nyadhifa zao mnamo wiki za hivi karibuni, katika mvutano wa kisiasa unaotokota kati ya Tshisekedi na Kabila ambao kwa miaka miwili iliyopita walikuwa na ushirikiano katika utawala wa nchi.