1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika UK apinga Trump kuhutubia bunge

7 Februari 2017

Spika wa bunge la Uingereza amesema rais wa Marekani Donald Trump hafai kualikwa kulihutubia bunge hilo wakati atakapofanya ziara rasmi nchini humo.

https://p.dw.com/p/2X5d4
Großbritannien Parlamentssprecher John Bercow in London
Spika wa bunge la Uingereza John BercowPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Dunham

Matamshi hayo ya Spika John Bercow yanaondoa uwezekano kwa Trump kupewa heshima hiyo wakati wa ziara yake baadae mwaka huu. Bercow aliwambia wabunge kwamba angepinga mwaliko huo hata kabla ya marufuku  ya Trump inayowazuwia raia kutoka mataifa saba yenye Waislamu wengi kuingia nchini Marekani.

"Kabla ya kuwekwa marufuku ya uhamiaji, binafsi ningepinga vikali kuruhusiwa rais Trump kutoa hotuba katika ukumbi wa Westminster. Baada ya kuwekwa kwa marufuku ya uhamiaji na rais Trump, ninapinga hata vikali zaidi hotuba ya rais Trump katika ukumbi wa Westminster," alisema Bercow bungeni siku ya Jumatatu.

Si matamshi ya kawaida

Matamshi ya Bercow hayakuwa ya kawaida kwa sababu maspika wa bunge la Uingereza wanatarajiwa kutoegemea upande wowote wa kisiasa. Ni mmoja wa maafisa wa bunge ambao wangekubali kumualika mgeni wa nje kuwahutubia wabunge.

USA Präsident Donald Trump
Rais Donal Trump anakosolewa kutoka kila kona ya dunia kutokana na mfumo wake wa utawala.Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Viongozi wa dunia waliowahi kupewa heshima ya kutoa hotuba kwa mabaraza yote ya bunge ni pamoja na Nelson Mandela, na mtangulizi wa Trump Barack Obama.

Bercow alishangiliwa na wabunge pale aliposema kwamba, inagwa Uingereza inathamini uhusiano wake na Marekani, "upinzani wetu dhidi ya ubaguzi wa rangi na kijinsia, na uungwaji wetu wa usawa mbele ya sheria na mahakama huru, ni mambo yenye umuhimu mkubwa zaidi.

Trump atazuru Uingereza kama mgeni wa Malkia, ziara iliotangazwa na waziri mkuu Theresa may alipomtembelea Trump mjini Washington mwezi uliopita.

Lakini baadhi ya raia wameonyesha mashaka na uharaka wa serikali kuwa karibu na rais huyo mwenye kuchochea mgawanyiko. waraka wa mtandaoni unaopinga ziara ya Trump umesainiwa na zaidi ya watu milioni 1.8, na utajadiliwa bungeni Februari 20.

Mpambano mahakani

Mahakama nchini Marekani zimesitisha kwa muda marufuku hiyo, na kuzusha maneno makali kutoka kwa rais huyo anaewasiliana kwa sehemu kubwa zaidi kupitia mtandao wa twita.

Mahakama ya rufaa mjini San Francisco leo itasikiliza hoja juu ya iwapo marufuku hiyo irejeshwe, kutoka kwa mawakili wa wizara ya sheria ya Marekani, na mawakili wa upande unaopinga kutoka majimbo ya Minnesota na Washington.

USA 9th Circuit Court of Appeals in San Francisco
Mahakama ya tisa ya rufaa ya Marekani mjini San Francisco, ambayo inasikiliza rufaa kuhusu marufuku ya uhamiaji ya Trump.Picha: Getty Images/J. Sullivan

Trump anasema hatua hizo zinalenga kulinda nchi dhidi ya kitisho cha ugaidi, na kumdhihaki Jaji James Robart aliesitisha marufuku hiyo, na ambaye aliteuliwa na Mrepublican mwenzake George W. Bush, akimueleza kama "anaejiita Jaji."

Benki Kuu Ulaya yaonya

Wakati huo huo, Benki Kuu ya Ulaya ECB imeelezea wasiwasi kuhusu hatua zinazopangwa kuchukuliwa na utawala wa Trump kulegeza sheria za udhibiti wa sekta ya benki, ikisema hatua kama hizo zilisaidia kusafisha njia ya mgogoro wa kifedha duniani.

Rais wa benki hiyo Mario Draghi alisema wakati wa kikao katika bunge la Ulaya, kwamba haoni sababu yoyote ya kulegeza sheria hizo zinazofahamika kama sheria za Dodd-Frank, ambazo zimepelekea kuwepo na sekta imara zaidi ya fedha kuliko ilivyokuwa kabla ya mgogoro wa mwaka 2007/2008.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtre.

Mhariri: Daniel Gakuba