SPD yarejea madarakani jimboni NRW
14 Mei 2012Japokuwa matokeo hayo yalitarajiwa , lakini nchi nzima ilikuwa inakodolea macho kwa shauku kubwa uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na uongozi mzima wa serikali ya kansela wa Ujerumani. Hilo hata hivyo si jambo geni. Jimbo la North Rhine Westphalia lina wakaazi milioni 18 na jimbo hilo linachangia kiasi ya robo ya pato jumla la taifa, na uchaguzi wa jimbo hilo mara zote huchukuliwa kama uchaguzi mdogo wa bunge la taifa.
Pamoja na hayo katika uchaguzi wa mwaka 1966, 1995 na 2005 , vyama vinavyounda serikali katika jimbo hili , viliingia madarakani katika uchaguzi mkuu wa taifa. Uchaguzi wa jana hata hivyo uliangaliwa kwa shauku hadi dakika ya mwisho kuweza kufahamu iwapo ushindi wa chama cha SPD ungeweza kutosha kuunda serikali pamoja na chama cha kijaniUlikuwa uchaguzi mgumu, ambao uliwahusu zaidi watu, amesema Kraft.
Katika furaha hiyo ya ushindi chama cha kijani kimechanganya pia na hali ya kujisikia ahueni. Chama hicho kwa mara nyingine tena kimefanikiwa kufanyakazi pamoja na SPD.
Uchaguzi uliotishwa na mapema katika jimbo hilo , umekipa chama cha CDU matokeo mabaya kabisa kuwahi kutokea katika jimbo hilo, chama hicho kikiambulia kiasi ya zaidi ya asilimia 26 tu kwa mujibu wa matokeo ya awali jana.
Ikiwa imebakia miezi 16 kabla ya kuingia katika uchaguzi wa taifa na Merkel kuwania kipindi cha tatu cha uongozi , kansela anakabiliwa na kazi ngumu ya kutathmini ni vipi anaweza kuhakikisha ushindi kwa chama chake cha CDU pamoja na kuhakikisha sera zake za kupambana na mzozo wa madeni katika eneo la euro zinatekelezwa.
Afisa mwandamizi wa CDU hata hivyo amekana kuwa kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi huo kutaathiri sera za kitaifa za chama hicho. Lakini hali hiyo ya kushindwa vibaya imemlazimu mgombea wa chama cha CDU Norbert Röttgen kuachia ngazi ya uongozi wa CDU katika jimbo hilo. Norbert amesema:
"Ni wazi tumeshindwa, ni machungu na inauma sana. Matokeo haya yananilazimu , kukabidhi madaraka ya uongozi wa chama cha CDU katika jimbo hili."
Nacho chama cha FDP mshirika mkuu katika serikali ya mseto ya kansela Merkel kimepata mtu maarufu ambaye hadi mwaka 2011 alikuwa katibu mkuu wa chama hicho Christian Lindner. Amefanikiwa kukivusha chama hicho na kupata zaidi ya asilimia 5 ya kura na kufanikiwa kuingia katika bunge.
Chama kipya cha Pirates kinashangiria kwa mara nyingine tena , kimefanikiwa kuingia katika bunge katika jimbo la nne sasa.
Mwandishi: Scholz, Kay-Alexander/ ZR/Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef