SPD kitayari kwa mazungumzo Ujerumani
24 Novemba 2017Haya ni baada ya mazungumzo ya Kansela Angela Merkel wa chama cha CDU na vyama vyengine kuvunjika wiki iliyopita. Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani amekuwa akikutana na viongozi wa vyama hivyo kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo hayo na Alhamis alikutana na kiongozi wa SPD, Martin Schulz.
Mazungumzo ya Steinmeier na Schulz yalidumu kwa zaidi ya saa moja ambapo alitarajiwa kumkumbusha kiongozi huyo wa upinzani kuhusiana na majukumu yake ya kisiasa kwa taifa, na kumshinikiza ili abadilishe msimamo wake kuelekea kuunda serikali nyengine ya muungano na wahafidhina.
Huenda kukaitishwa uchaguzi mpya iwapo mazungumzo hayatozaa matunda
Kabla mkutano huo, Schulz alionekana kulegeza msimamo wake ingawa alikataa katakata kurudi katika serikali iliyopo ya muungano pamoja na Merkel, baada ya chama chake kupata matokeo mabaya katika uchaguzi wa Septemba.
Chama cha Schulz kimekuwa katika serikali ya muungano tangu mwaka 2013, ila Schulz amesema chama hicho ni sharti kifuate wanachotaka wapigakura kwa kuwa wapinzani. "Tunafikiri ni muhimu kwa raia wa nchi hii na hapa namaanisha wapigakura, waweze kuangazia upya hali hii," alisema Schulz. "Hatuogopi uchaguzi mpya. Kutokana na matokeo ya ule uchaguzi wa Septemba 24, hatuko tayari kuingia katika serikali ya mseto," aliongeza kiongozi huyo.
Iwapo juhudi za kuunda serikali ya mseto zitagonga mwamba, huenda kukaitishwa uchaguzi mpya, jambo ambalo wanasiasa wengi wa SPD hawaliungi mkono, kwani chama chao kilipata matokeo mabaya kabisa kuwahi kupata kihistoria kwenye uchaguzi uliopita.
Huku hayo yakiarifiwa, mmoja wa wanachama wa ngazi za juu katika chama hicho cha SPD amekwenda kinyume na kauli ya Schulz na kusema wako tayari kufanya mazungumzo na vyama vyengine, ili waukwamuwe mkwamo wa kisiasa uliopo. Iwapo hilo litafanyika basi hakutokuwa na haja ya uchaguzi mpya kufanyika.
Chama cha SPD kiko tayari kwa mazungumzo
Katibu Mkuu wa SPD, Hubertus Heil, amesema, "hatutosema la, kwa mazungumzo," mwisho wa kunukuu. Lakini Heil hakusema iwapo chama hicho kitafanya mazungumzo na vyama gani au ikiwa wanalenga kuwepo katika serikali ya muungano au kama wataiunga mkono serikali iliyo na wabunge wachache inayoongozwa na Angela Merkel.
Kansela Merkel mwenyewe alisema mapema wiki hii kwamba angependelea uchaguzi wa mapema kuliko hali ya kutoeleweka ya serikali yenye wabunge wachache katika bunge la Ujerumani.
Merkel anakabiliwa na mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa tangu kushindwa kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto. Suala hilo limeibua wasiwasi kote Ulaya kuhusiana na hali ya ati ati iliyochukua muda mrefu katika nchi hii iliyo na nne kwa uchumi mkubwa zaidi duniani.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/DPAE/APE
Mhariri: Mohammed Khelef